Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) Mhe. Selemani Jafo amewataka wananchi wa kijiji cha Manzase, kuhakikisha kuwa wanautunza mradi wa maji ulioanzishwa kwa gharama yoyote.
Akizungumza na wananchi wa kijiji cha Manzase Wilaya ya Chamwino, wakati wa ziara aliyoifanya ya kukagua mradi wa maji Mheshimiwa Jaffo alisema iwapo wananchi hao watautunza mradi huo vizuri utawasaidia zaidi kwani wamepata taabu ya maji kwa kipindi kirefu sana.
“ Kumekuwa na kawaida ya baadhi ya wananchi katika maeneo mbalimbali ambapo miradi ya namna hii imekuwa ikianzishwa kwa makusudi kabisa, wanaiharibu miundo mbinu ya miradi hii kwa kukata mabomba kwa makusudi kwa lengo la kunywesha mifugo, kuiba vifaa mbali mbali kwenye mabomba na kuiba mitambo inayosaidia kusukuma maji” Alisisitiza Mhe. Jafo.
Aidha, aliwataka Viongozi wote wa kijiji hicho kuhakikisha kuwa kamati ya maji ya kijiji ambayo ndicho chombo maalumu cha kusimamia maji katika ngazi ya kijiji kinasimamiwa ipasavyo kwani kumekuwa na tabia ya baadhi ya viongozi hao kujimilikisha miradi hiyo kwa kutumia fedha zinazokusanywa kwa matumizi yao wenyewe, na pindi miundo mbinu inapoharibika kijiji kinakosa fedha za kupatra marekebisho.
Diwani wa kata ya Manzase Mh. Steven Kwanga alisema, mradi huo wa maji utasaidia sana katika ukuaji wa uchumi wa wananchi wake kwani wamekuwa wakitumia muda mwingi kutafuta huduma ya maji, vilevile wananchi wamekuwa wakitumia kiasi kikubwa cha fedha kununua maji badala ya fedha hiyo ingetumiwa kutimiza mahitaji mengine.
Mradi huo wa maji wa kijiji cha Manzase unatarajiwa kuzinduliwa wakati wowote mwezi huu kwani mkandarasi wa mradi huo akishirikiana na Ofisi ya Rais TAMISEMI amekwisha ukamilisha kwa kiasi kikubwa na unatarajiwa kuhudumia idadi ya watu wasiopungua 8000.
Katika ziara hiyo Mhe. Jafo alikuta Idadi kubwa ya watoto walioandikishwa kujiunga na darasa la kwanza hali iliyopelekea kukosekana kwa vyumba vya kutosha kwa ajili ya kujifunzia wanafunzi ambapo kwa kutatua kero hiyo, shule hiyo imeanza ujenzi wa vyumba vya madarasa na kwa upande wake alichangia bati 164 ili kuwezesha madarasa hayo kukamilika.
Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino
Sanduku la posta: 1126 Dodoma
Simu ya Mezani: 026 296 1511
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@chamwinodc.go.tz
Hakimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino. Haki zote Zimehifadhiwa.