Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ametoa rai kwa viongozi kutambua wajibu wa kutekeleza Dira ya Taifa 2050 na mipango ya maendeleo ya sekta ya kilimo ambayo imedhamiria kuongeza kasi ya ukuaji wa kilimo hadi kufikia asilimia 10 kwa mwaka ifikapo 2030 na kuendelea.
Makamu wa Rais ametoa rai hiyo wakati akifungua maonesho na sherehe za Wakulima maarufu kama Nanenane zinazofanyika kitaifa katika viwanja vya Nzuguni Mkoani Dodoma. Amesema ni vema viongozi kuwajibika kuwaelekeza wakulima , wafugaji na wavuvi kuweka nguvu zaidi kwenye mazao yenye thamani kubwa sokoni, kuwekeza katika uzalishaji wa kisasa ili kukidhi mahitaji ya soko la ndani na nje, kuvutia uwekezaji wa ndani na nje pamoja na kuwekeza katika miundombinu baridi ya uhifadhi na usafirishaji.
Ameongeza ni vema viongozi kuhamasisha uwekezaji mkubwa katika teknolojia za kisasa za kilimo, ikiwemo kilimo janja, uwekezaji katika umwagiliaji, upatikanaji wa fedha na mitaji, kutafuta masoko ya uhakika na kuhakikisha wanajiimarisha zaidi katika kilimo-biashara.
Pia Makamu wa Rais amesema ni inapaswa viongozi kusimamia uwezeshaji wa wakulima, wafugaji na wavuvi kiuchumi, hususani upatikanaji wa mitaji, teknolojia, elimu na mafunzo pamoja na upatikanaji wa huduma za ugani, ikiwemo kukuza matumizi ya kanuni bora za kilimo. Halikadhalika kuhamasisha maendeleo ya ushirika na ushirikiano kati ya wakulima, wafugaji, wavuvi na watafiti, maafisa ugani na watunga sera.
Vilevile Makamu wa Rais amesema ni wajibu wa viongozi kuhimiza Wananchi kutumia mbinu zinazoweza kuhimiri athari zitokanazo na mabadiliko ya tabianchi na changamoto nyingine zinazowakumba wakulima ikiwemo kuhimiza matumizi bora ya ardhi, kushawishi wananchi kupanua mawanda ya kilimo na kuhimiza zaidi kilimo cha mazao yanayohimili ukame.
Makamu wa Rais ametoa wito kwa viongozi kutoa elimu kwa wakulima, wafugaji, wavuvi na wasindikaji wa mazao ya kilimo, mifugo na uvuvi kuhusu fursa zilizopo na kupata mitaji kutoka kwenye benki na taasisi zingine za fedha ambazo tayari zinatoa mikopo nafuu kwa ajili ya kilimo-biashara
Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino
Sanduku la posta: 1126 Dodoma
Simu ya Mezani: 026 296 1511
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@chamwinodc.go.tz
Hakimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino. Haki zote Zimehifadhiwa.