Katibu tawala (DAS) wilaya ya Chamwino ndugu Neema Nyalege amefanya kikao cha robo ya nne ya utekelezaji wa mkataba wa lishe ngazi ya kata. Kikao hicho kimefanyika Agosti 21, 2025 katika Ukumbi wa Halmashauri ambapo kamati ya utekelezaji wa mkataba huo imethibitisha muhtasari wa ajenda za kikao kilichopita na kupokea ripoti ya utekelezaji wa mkataba wa afua za lishe kwa ngazi ya kaya na shule za msingi na sekondari.
Nyalege amepongeza kamati hiyo kwa kutekeleza kwa ufanisi mkubwa mikakati ya afua za lishe kwa kipindi cha robo ya nne ya mwaka wa fedha 2024/2025 na kuwezesha kata zote kupata alama za kijani ya utekelezaji wa mkataba huo. Aidha, amesisitiza kuendelezwa kwa juhudi hizo ili kupata matokeo makubwa zaidi.
“Najua tunafanya vizuri na ninawapongeza kwa hilo, lakini bado tuna kazi ya kufanya. Tuone namna ya kutumia wale waliokuwa vinara katika utekelezaji wa mkataba huu kuendelea kutoa elimu kwa maeneo ambayo hawafanyi vizuri, ili mambo yetu yawe mazuri zaidi”.
Naye Afisa Lishe Rahel Magafu, ameelezea mafanikio yaliyofikiwa katika robo ya nne ya utekelezaji wa mkataba wa lishe ngazi ya kata kuwa ni pamoja na ongezeko la wanafunzi wanaopata chakula kwa shule za msingi na sekondari kutoka 42.7% hadi 80.7%, Vijiji na kata zote kubandika taarifa za lishe katika mbao za matangazo, na wahudumu wa afya ngazi ya jamii kufikia kaya 13,204 ikiwa ni zaidi ya lengo la kaya 8072.
Mafanikio mengine ni kufanyika kwa maadhimisho ya siku ya afya na lishe katika kata na vijiji vyote, Vijiji na kata zote kuwa na kanuni za lishe, pamoja na kupima hali ya lishe ya watoto ambapo jumla ya watoto 17031 walipimwa ikiwa ni zaidi ya lengo lilikokuwa limewekwa la kupima watoto 8072. Hata hivyo ameeleza kuwa watoto 31 waliobainika kuwa na utapiamlo mkali walipewa rufaa ya matibabu.
Aidha, ameeleza kuwa miongoni mwa changamoto zinazokabili utekelezaji wa mkataba wa lishe ngazi ya kata ni muitikio mdogo wa wanaume katika kushiriki shughuli na mikakati ya kutekeleza afua za lishe ikiwemo maadhimisho ya siku ya afya na lishe.
Kwa upande mwingine amempongeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino kwa kutoa fedha za mapato ya ndani sh. 135,253,600 sawa na 100% ya fedha zilizoombwa ili kutekeleza afua za lishe kwa mwaka 2024/2025, pamoja na kutoa zawadi ya cheti na fedha taslimu kwa kata na shule vinara katika utekelezaji wa mkataba wa lishe kwa robo ya nne.
Kata hizo ni Makangw’a (mshindi wa kwanza), Msanga (mshindi wa pili) na Manda (mshindi wa tatu), huku shule zikiwa Shule ya Msingi Mizengo Pinda na Shule ya Sekondari Itiso.
Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino
Sanduku la posta: 1126 Dodoma
Simu ya Mezani: 026 296 1511
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@chamwinodc.go.tz
Hakimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino. Haki zote Zimehifadhiwa.