Kamishna wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Asina Omari, ametembelea mafunzo ya siku tatu kwa wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ngazi ya Kata (ARO Kata) Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino ambayo yamehitimishwa leo Agosti 6, 2025 katika Wilaya ya Chamwino.
Akizungumza katika ziara yake hiyo amewasisitiza wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ngazi ya Kata, Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino kuzingatia viapo walivyoapa kabla ya kuanza kwa mafunzo hayo, hivyo amewataka kuviishi viapo hivyo kwa vitendo wakati wa utekelezaji wa majukumu yao.
Pia Kamishna. Asina amewataka watendaji hao wa uchaguzi kuzingatia utaratibu uliowekwa wa utoaji na upokeaji wa taarifa za masuala mbalimbali ya uchaguzi, hivyo amewataka kuepuka kupokea maelekezo kutoka kwa mtu au taasisi ambayo haihusiki na uchaguzi ispokuwa Tume huru ya Taifa ya Uchaguzi.
Halikadhalika, Kamishana. Asina amewasisitiza washiriki wa mafunzo hayo kuhakikisha hawatoi upendeleo kwa wagombea au chama chochote cha siasa kinachoshiriki uchaguzi katika hatua mbalimbali za uchaguzi
“Kuviishi na kuheshimu viapo mlivyoapa ni kutofanya upendeleo wa aina yeyote kwa wagombea au vyama vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi katika hatua mbalimbali, iwe kwenye kutoa fomu, kwenye uteuzi, kwenye kampeni hadi hatua ya kutangaza matokeo, epuka upendeleo”. Alisisitiza Kamishna Asina.
Kwa upande wa Mratibu wa Uchaguzi Mkoa wa Dodoma Ndg. Jofrey Evarist Pima amewaasa wasimamizi hao wa uchaguzi ngazi ya kata kutekeleza majukumu yao kwa uaminifu, uadilifu na weledi pamoja na kuzingatia katiba ya nchi, sheria ya uchaguzi, kanuni, miongozo pamoja na maelekezo ambayo tayari yametolewa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi.
Aidha, amewahimiza kutotekeleza majukumu yao ya uchaguzi kwa mazoea na uzoefu bali tu kwa sheria, kanuni, miongozo na maelekezo ya Tume.
Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino
Sanduku la posta: 1126 Dodoma
Simu ya Mezani: 026 296 1511
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@chamwinodc.go.tz
Hakimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino. Haki zote Zimehifadhiwa.