Mkuu wa Wilaya ya Chamwino Mhe. Janeth Mayanja, leo Oktoba 10, 2025 amekabidhiwa na taasisi ya ELICO vyombo vya usafiri, na vifaa mbalimbali vya TEHAMA; ikiwa ni pamoja na pikipiki tatu za umeme, baiskeli moja ya umeme, kompyuta tatu, printa tatu na vifaa vya kutunza umeme (UPS) tatu kwa ajili ya zahanati ya Chitabuli, Chiwondo, Mafurungu, na Mahamha.
Akizungumza wakati wa makabidhiano yaliyofanyika katika zahanati ya Mahamha, Mhe. Mayanja amemshukuru Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi ya ELICO Ndg. Sisty Basil kwa kuona haja ya kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuboresha huduma za afya katika Wilaya ya Chamwino.
“Tunakushukuru kwa kuichagua Wilaya ya Chamwino, kwani mngeweza kuchagua wilaya nyingine yoyote ya mkoa wa Dodoma, lakini imewapendeza kuichagua wilaya ya Chamwino, na kuunga juhudi za serikali katika kuboresha huduma za afya katika Wilaya hii.”
Vilevile Mhe. Mayanja amempongeza Kaimu Mkurugenzi na Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino Dkt. Euseby Kessy, kwa namna ambavyo anafanya kazi na wadau wa maendeleo hasa taasisi zisizo za kiserikali zinazojitokeza kuunga mkono juhudi za serikali katika kuboresha huduma za afya katika wilaya ya Chamwino.
Kadhalika, Dkt. Kessy ameshukuru taasisi ya ELICO kwa kuanzisha ushirikiano na serikali, na kuwezesha upatikanaji wa vitendea kazi mbalimbali katika sehemu za kutolea huduma za afya, hasa zahanati mpya.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, Mganga Mfawidhi wa zahanati ya Mahamha Dkt. Martin Dorothei Mluge na Mganga Mfawidhi wa zahanati ya Chiwondo, Dkt. Lucy Mushi wamesema kwamba kuwepo vitendea kazi hivyo kutaboresha huduma za afya katika zahanati zao hasa huduma ya mkoba na utunzaji wa taarifa.
Mbali na vifaa vilivyokabidhiwa leo, taasisi ya ELICO imejenga visima vya maji vitatu, ikiwa ni kimoja kimoja katika hospitali ya Wilaya ya Chamwino, Zahanati za Chitabuli na Mafurungu, pamoja na kuvifungia pampu zinazotumia umeme wa jua. Pia, taasisi hiyo imefunga mifumo ya umeme wa jua katika zahanati zote nne ambazo ni wanaufaika wa vitendea kazi vilivyokabidhiwa leo.
Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino
Sanduku la posta: 1126 Dodoma
Simu ya Mezani: 026 296 1511
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@chamwinodc.go.tz
Hakimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino. Haki zote Zimehifadhiwa.