Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Khamis Hamza Khamis ameongoza zoezi la upandaji miti lililofanyika leo Mei 26, 2023 shule ya sekondari Buigiri.
Taasis zilizohisani zoezi hili ni TCCHP ikishirikiana na Habari Conservation Chini ya ufadhili wa TFS - PMM Living way.
Akizungumza nawananchi Mhe. Khamis Hamza Hamis amewahimiza wadau wote wa mazingira hususani waandishi wa habari kuendelea kutoa elimu ya mazingira.
" Wanahabari tumieni weledi wenu kuwaelimisha wananchi umuhimu wa kutunza mazingira na athari zake," alisema.
Vilevile aliendelea kusema kuwa ipo haja ya kuendelea kutoa elimu ya kuepuka mabadiliko ya tabia ya nchi kwa kuunga juhudi za Serikali.
" Tupandeni miti mingi na kuitunza, tumeshazindua kampeni maalum mashuleni ya kusomana kupanda miti." Alisema Naibu Waziri.
Aidha Naibu Waziri alizungumzia kuhusu suala la biashara ya hewa ukaa ambapo alieleza kuwa bado jamii haijawa na uelewa juu yake na kuelekeza kuwa elimu iendelee kutolewa kuhusiana na biashara hiyo.
"Biashara ya hewa ukaa, bado jamii haijajua taaluma hii, hivyo naomba mkawape taaluma wananchi wetu, moja namna ya kujua fursa na namna gani ya kunufaika na biashara hii na watu wa habari mnayo nafasi kubwa ya kuelimisha jamii," alisema Naibu Waziri.
Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Muungano na mazingira alizungumzia suala la uelewa mdogo wa wananchi katika kutunza vyanzo vya maji na kueleza kuwa hakuna mazingira bila maji, na ndio maana siku hizi wanashuhudia wanyama wakitangatanga kwenye makazi ya watu wakitafuta maji. Alielekeza shughuli za kibinadamu kwenye vyanzo vya maji kama vile kilimo, kunywesha mifugo na uchimbaji madini zidhibitiwe.
Vilevile alizungumzia suala la kuwasaidia watu wenye ulemavu hususani wenye ulemavu wa ngozi ( ualbino) pamoja na viungo kwa kupanda miti kwa maana wanapata tabu na jua kali.
Jumla ya miti 1,000 imepandwa ambapo miti ya matunda ni 700 na ya kivuli 300. Mhe. Naibu Waziri amesisitiza miti hiyo itunzwe vizuri ili ikue.
Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino
Sanduku la posta: 1126 Dodoma
Simu ya Mezani: 026 296 1511
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@chamwinodc.go.tz
Hakimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino. Haki zote Zimehifadhiwa.