Wakati wakulima wakisherehekea siku ya Nane Nane mkoani Dodoma, Msanii Nassib Abdul maarufu kama Diamond Platnumz amefanya ziara kwenye mashamba ya zabibu yaliyopo Dodoma ikiwa ni sehemu ya kuhamasisha utalii wa ndani.
"Najisikia furaha kutangaza mema ya nchi yangu na hasa zabibu za Dodoma kwa kuwa ndio eneo lenye zabibu zenye ubora wa juu sana duniani. Nitatumia sanaa yangu kuhakikisha ninaunga mkono juhudi za Rais Magufuli kwa kuifanya dunia kujua utajiri wa vivutio vya utalii Mungu alivyotujaalia" Alisema Diamond.
Diamond ameyasema hayo alipokuwa eneo la Nkhulabi, Kata ya Mpunguzi alipotembelea mashamba ya zabibu na kujionea shughuli za uzalishaji wa mvinyo katika kiwanda cha usindikaji mvinyo cha Dane Holdings Co. Ltd kinachomilikiwa na Eng.Danford Semwenda.
Katika ziara hiyo Diamond aliambatana na Wabunge Livingstone Lusinde (jimbo Mtera-Chamwino) na Mh Anthony Mavunde (jimbo la Dodoma) wamewataka wananchi wa Dodoma kuchangamkia kilimo cha zabibu kwani muda sio mrefu mahitaji ya zabibu yatakuwa makubwa hasa kutokana na Serikali ya awamu ya Tano chini ya Rais Magufuli kwa kushusha tozo ya mchuzi wa zabibu kutoka Tsh 3315 mpaka Tsh 450 na kumshukuru Diamond kwa kuamua kuitangaza zabibu ya Dodoma kwa kushirikiana na Bodi ya Utalii Tanzania (TTB).
Aidha Mkuu wa Wilaya wa Bahi Mh. Mwanahamis Mukunda kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, amempongeza Msanii Diamond kwa kuwa mfano kwa wasanii wengine katika kutangaza vivutio vya utalii nchini na kumuomba mwanamuziki huyo kushirikiana na uongozi wa serikali ya Mkoa wa Dodoma kwa kulitangaza Tamasha la Mvinyo Wine Festival 2019 kwa kuwa mkoa wa Dodoma umejipanga kurudisha heshima ya zao la zabibu.
Wilaya ya Chamwino ni moja ya Wilaya za Mkoa wa Dodoma zinazolima zao la zabibu kwa wingi.
Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino
Sanduku la posta: 1126 Dodoma
Simu ya Mezani: 026 296 1511
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@chamwinodc.go.tz
Hakimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino. Haki zote Zimehifadhiwa.