Mkuu wa Wilaya ya Chamwino Mhe. Gifty Isaya Msuya, 15 Mei 2023 amekagua maendeleo ya mradi wa ujenzi wa shule ya msingi mpya yenye mikondo miwili inayojengwa katika kijiji cha Mjelo, unaotekelezwa kwa fedha za mradi wa Boost.
Mhe. Gifty amesema shule hiyo ilikuwa ni shule shikizi iliyojengwa kwa nguvu za wananchi kwa kujenga darasa la awali na darasa la kwanza .
Hata hivyo ameishukuru Serikali ya awamu ya sita kwa kukipatia kijiji hicho kiasi cha fedha shilingi milioni 490 kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 14, ofisi ya utawala na matundu 24 ya vyoo.
“Ndugu zangu wa Mjelo sisi tumekuja kuangalia maendeleo ya mradi ni dhahiri kwamba tangu kipindi cha Uhuru miaka 60 ya Uhuru iliyopita ambapo kijiji hiki kilikuwa kimoja cha Handali na baadae tukagawanyika na kupata Mjelo na Handali, lakini kwa kipindi tangu mimi nimefika kumekuwa na malalamiko kwamba shule ya msingi Handali imeelemewa inawanafunzi wengi, majengo machache, lakini eneo pia ni dogo na malalamiko haya tumekuwa tukipokea kupitia vikao mbalimbali.”
“Nimeambiwa hapa kuna shule shikizi darasa la awali na darasa la kwanza ambao wanasomea hapa na sisi tukaona katika utaratibu huu ambao Mhe. Rais ametoa fedha nyingi za kujenga madarasa tukaomba kupitia Mbunge wenu, viongozi wa kata, Waheshimiwa Madiwani, wakawasilisha maombi kwamba tupatiwe shule nyingine pacha na sisi tukaona ni wazo zuri, tukaomba fedha hizi TAMISEMI natukafanikiwa kupata milioni 490 katika eneo hili ambapo yatajengwa madarasa 14, ofisi ya utawala, na matundu 24 ya vyoo “, alisema Mkuu wa Wilaya.
Vilevile Mhe. Gifty amewasisitiza wananchi kushiriki katika utekelezaji wa miradi hiyo kwa kujitolea nguvu kazi ili kuhakikisha miundombinu inajengwa kwa ukamilifu.
Alisema wanachi watakaposhiriki itasaidia kuhifadhi fedha nyingine kwaajili ya kukarabati madarasa ambayo yalijengwa kwa nguvu za wananchi.
“Sasa Serikali ya Mhe. Samia Suluhu Hassani inatoa mabilioni lakini katika kutoa fedha hizi haitaki wanachi wabaki nyuma lazima wananchi wajue kinachoendelea lakini washiriki moja kwa moja kwenye kuhakikisha miundombinu hii inajengwa kwa ukamilifu, lakini fedha inayotumika inatumika vizuri na nguvu kazi inatakiwa wananchi wachimbe msingi, wakusanye kokoto, mawe na bahati nzuri tumejaliwa mchanga huku Handali na Mjelo, tukusanye mchanga ili tupunguze gharama za mradi,”
“ Inaonekana hapa wanchi kujitoa ni shida, kwa hiyo wananchi mnapaswa kujitoa ili shule yetu iwe ya mfano. Lazima zifanane isiwe kule kuna madarasa mazuri huku kuna magofu haitopendeza. Tunahitajika tutoe nguvu kazi ili tusiweke hela nyingi kwenye hizi kazi ambazo tunaweza kufanya kwa mikono yetu, ili pesa zielekezwe kwenye vitu vinavyotoka viwandani zaidi.” Alisema.
Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino
Sanduku la posta: 1126 Dodoma
Simu ya Mezani: 026 296 1511
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@chamwinodc.go.tz
Hakimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino. Haki zote Zimehifadhiwa.