Katbu Tawala wa Mkoa wa Dodoma ndugu Fatuma Mganga ametoa pongezi kwa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino kwa kupata hati safi kwenye ukaguzi wa hesabu za mwaka wa fedha 2020/2021.
Pongezi hizo amezitoa kwenye kikao cha Baraza la Madiwani la kupitia hoja za Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa wa Hesabu za Serikali (CAG) kilichofanyika leo Juni 23, 2022 kwenye Bwalo la Chamwino Sekondari.
Aidha Katibu Tawala wa Mkoa amepongeza juhudi zilizofanyika za kufunga hoja 07 za mwaka wa fedha 2020/2021 kati ya hoja 27 na kufuta hoja 36 za miaka ya nyuma.
Sambamba na pongezi hizo amewataka Wataalam wanaohusika na hoja kuhakikisha wanazipatia majibu mapema hoja zote zilizobaki ili ziweze kufungwa na hivyo kuondokana na kuwa na mlundikano wa hoja zisizo za lazima.
"Twendeni tukajibu hizi hoja, kuna tabia tukimaliza vikao hivi tunafunga kitabu mpaka tena karibu na CAG anapokuja ndio tunaanza kutafuta majibu. Hatuwezi kupata majibu, majibu mengine yanapaswa yaanze kufanyiwa kazi mapema. Tusipojiwekea mkakati sasa tutakuja kukumbuka wakati CAG anakuja ambapo tunakuwa hatuna muda."
Vilevile Katibu tawala wa Mkoa ameipongeza Halmashauri kwa kuanzisha mradi mkubwa wa kilimo( block farming) utakaoiwezesha Halmashauri kuongeza mapato na kuitaka Halmashauri iendelee kubuni vyanzo vingine vipya vya mapato vitavyoiwezesha kujiendesha yenyewe pasipo kusababisha madeni ya ndani.
Pamoja na hayo Katibu Tawala Mkoa amesisitiza suala la wataalamu wa Halmashauri kutunza vizuri kumbukumbu za nyaraka kwani utunzaji hovyo wa nyaraka hizo hupelekea upotevu ambao matokeo yake ni kutengeneza hoja.
Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino
Sanduku la posta: 1126 Dodoma
Simu ya Mezani: 026 296 1511
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@chamwinodc.go.tz
Hakimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino. Haki zote Zimehifadhiwa.