Tarehe 19 Juni 2019, Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa-TAMISEMI Mheshimiwa Seleman Jafo ametembelea eneo la Ujenzi wa Hospitali ya Uhuru na kuagiza uongozi wa Serikali ya Mkoa na Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino kuhakikisha ujenzi huo unaanza ndani ya siku saba.
Ikumbukwe kuwa Jumanne ya Novemba 20, 2018 Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, alitoa tangazo la maagizo ya Mh. Rais Magufuli yaliyooelekeza kiasi cha Sh milioni 995.182 zilizokuwa zimetengwa kwa ajili ya kufanikisha sherehe za Uhuru Desemba 9 mwaka jana, zitumike kwa ajili ya ujenzi wa hospitali hiyo wilayani Chamwino ambayo itakuwa ya kisasa na teknolojia za hali ya juu zitatumika kutoa matibabu. Hata hivyo Serikali imetenga fedha nyingi zaidi kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa ujenzi wa Hospitali hii.
Katika ziara hiyo ambayo waziri aliambatana na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Bilinith Mahenge waziri Jafo alipata fursa ya kuzungumza na watumishi wa Halmashauri ya Chamwino na kuwataka watumishi kushirikiana na kudumisha upendo miongoni mwao.
Aidha Mh. Waziri amempongeza Mkurugenzi wa Halmashauri Bw. A. H. Masasi na watumishi wote kwa kutii agizo la kuhamia kwenye ofisi mpya za Halmashauri ya Chamwino zilizopo eneo la Buigiri.
“Nimefurahishwa sana kuona sasa watumishi mmehamia katika ofisi zenu. Niagize tena SUMA-JKT kuhakikisha ndani ya mwezi mmoja wanakamilisha kazi zao za msingi katika jengo hili”. Alisema Mh. Jafo
Vilevile Mh. Jafo ameitaka Halmashauri kuongeza kasi ya upimaji wa viwanja ili kuhakikisha Chamwino ambapo ni makazi ya Rais panapangika vizuri na kusema kuwa upimaji wa viwanja utaongeza thamani ya ardhi na itaiongezea mapato Halmashauri. Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri Bw. Masasi amueleza waziri kuwa ameshapokea kiasi cha shilingi mil. 500 kwa ajili ya kutekeleza zoezi la upimaji wa viwanja.
Akitoa neno la Shukrani, Mwenyekiti wa Halmashauri Mh. Samwel A. Kaweya amemshukuru waziri na kuahidi kuwa madiwani watashirikiana na wataalam kuhakikisha maagizo yote yanatekelezwa.
Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino
Sanduku la posta: 1126 Dodoma
Simu ya Mezani: 026 296 1511
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@chamwinodc.go.tz
Hakimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino. Haki zote Zimehifadhiwa.