Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma kwa kushirikiana na Agricultural Marketing Development Trust wamefanya kikao na wakuu wa Idara za Uwekezaji, viwanda na biashara, Idara ya kilimo, umwagiliaji na Ushirika pamoja na wawakilishi wa wafanyabiashara na wakulima Halmashauri ya wilaya ya Chamwino chenye lengo la kuandaa mkakati wa kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji mkoa wa Dodoma.
Kikao kimefanyika Agosti mosi, 2023 kwenye ukumbi wa Halmashauri ambapo wajumbe waliwasilisha na kujadili changamoto mbalimbali zinazokwaza uwekezaji ndani ya wilaya ya Chamwino.
Akizungumza kwenye kikao hicho alipokuwa anawakaribisha wageni Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Chamwino Dkt. Semistatus H. Mashimba amewashukuru Mkuu wa Mkoa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma kwa ujio wa wageni hao, pia amewakaribisha na kuwaomba kuichukulia Chamwino kwa jicho la kipekee kwani Halmashauri hii ndio makazi ya Mhe. Rais, hivyo miradi na mambo yanayotekelezwa yanapaswa kuwa ya kiwango juu.
Aidha alisema Halmashauri ya Chamwino ipo kwenye mlengo huohuo wa kufanya wekezaji kwenye sekta ya kilimo na mifugo. Aliwakaribisha kwenye Mkutano maalum wa wadau kwa ajili ya kuanzisha Jukwaa tendaji la kilimo, mifugo na Ardhi unaotarajiwa kufanyika Agosti 4, 2023 kwenye Ofisi za Halmashauri.
Sambamba na hayo Dkt. Mashimba alishauri wataalam hao waweze kuangalia ni kwa namna gani wanaweza kuanzisha utalii wa Ikulu.
"Nashauri kwenye fursa za uwekezaji mnaweza kuangalia ni namna gani tunaweza kutengeneza utalii wa Ikulu, kwa maana kwenye hii Wilaya ni lazima tuwe na utalii wa eneo husika maana ninyi ni wataalamu wa mambo haya." Alisema Dkt. Mashimba.
Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino
Sanduku la posta: 1126 Dodoma
Simu ya Mezani: 026 296 1511
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@chamwinodc.go.tz
Hakimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino. Haki zote Zimehifadhiwa.