Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR - TAMISEMI) Mhe. Selemani Jafo amewataka Wakandarasi nchini kutimiza wajibu wao na kutekeleza miradi wanayopewa na Mamlaka za Serikali nchini kwa wakati, uaminifu na kuacha ubabaishaji.
Akizungumza katika uzinduzi wa mradi wa maji katika kijiji cha Wilunze wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma, Mheshimiwa Jafo amesema mkandarasi yeyote atakayepewa tenda ya mradi katika halmashauri yoyote nchini na asiitekeleze kwa wakati hataweza kupewa tenda mahali popote pale nchini.
“Kumekuwa na uzembe kwa Wakandarasi nchini, mkandarasi anapewa kazi ya kujenga daraja, kujenga visima vya maji, barabara au mradi mwingine wowote katika halmashauri, badala ya kutekeleza mradi huo kwa wakati ili wananchi waendelee kupata huduma hiyo, yeye analeta uzembe na ubabaishaji, mtu wa namna hiyo hatutamvumilia katika serikali hii” Alisisitiza, Mhe. Jafo.
Aidha, aliwataka wanakijiji wa Wilunze kuulinda mradi huo wa maji kwa kila mmoja kuwa msimamizi wa mradi na kuutaka Uongozi wa kijiji hicho kuhakikisha kuwa kinaundwa chombo cha watumiaji wa maji kijijini hapo ambacho kitakuwa na wajibu wa kusimamia mradi huo.
Mradi wa maji wa kijiji cha Wilunze uliozinduliwa leo ni mmoja kati ya miradi ya maji ya vijiji kumi inayojengwa wilayani Chamwino kupitia Programu ya Maji Vijijini. Mradi huo uliojengwa na Mkandarasi M/S Kijima Contractors akisimamiwa na Ofisi ya Mhandisi wa maji wilaya ya Chamwino umegharimu jumla ya sh. 347,909,621.
Kwa upande wake Mbunge wa Chilonwa Mhe.Joel Mwaka amemshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri na Serikali kwa ujumla kwa kuwapatia huduma ya maji safi wananchi wake na kuwasisitiza wananchi kuuliunda mradi huo kwa hali na mali kwani umeigharimu Serikali kiasi kikubwa cha fedha katika utekelezaji wake
Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino
Sanduku la posta: 1126 Dodoma
Simu ya Mezani: 026 296 1511
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@chamwinodc.go.tz
Hakimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino. Haki zote Zimehifadhiwa.