Uzinduzi wa bonanza la walimu Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino Mkoani Dodoma, bonanza hilo limeandaliwa na Tume ya utumishi wa walimu - TSC Wilayani Chamwino mkoani Dodoma.
Naibu katibu Mkuu, Elimu Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa Dkt. Charles Msonde amezindua bonanza la michezo la walimu lililoandaliwa na Tume ya utumishi wa waalimu TSC Wilayani Chamwino mkoani Dodoma, lenye lengo la kuwakutanisha walimu wa shule za msingi na sekondari wilayani humo kupitia michezo.
Akiwa mgeni rasmi katika TSC bonanza 2023 lililofanyika katika shule ya sekondari Chamwino Disemba 2, 2023 Dkt. Msonde aliwatoa hofu walimu juu ya utatuzi wa changamoto za walimu zinazohusisha kupandishwa madaraja, kulipwa fedha za uhamisho na changamoto zinginezo zinazoweza kufifisha ustawi wa waalimu.
Alisema kwa sasa Serikali inaendelea na mchakato wa kuhakikisha stahiki za waalimu zinashughulikiwa kwa wakati na usahihi ili kuinua ari na motisha za walimu katika utekelezaji wa majukumu yao ili kuboresha upatikanaji wa elimu bora kwa wanafunzi wa wilaya ya Chamwino na Tanzania kwa ujumla.
Pia amesema msingi wa utekelezaji wa mkakati huo unalenga kupandisha ufaulu wa wanafunzi mashuleni baada ya kubaini kuwa ari na motisha ya waalimu iko chini kufuatia changamoto za kimaslahi zinazowakabili jambo linalosababisha baadhi ya wanafunzi kufika darasa la tatu bila kujua kusoma na kuandika.
Pia ametoa wito kwa walimu kutekeleza wajibu wao ipasavyo ili kuboresha elimu wakati ambapo Serikali inaendelea kutekeleza mkakati wa kufanya uhakiki wa mapitio ya stahiki zao . zoezi linalofanywa kupitia tume ya utumishi wa waalimu TSC ili kuhakikisha hakuna mwalimu anayezidishiwa ama kupunguziwa stahiki zake kulingana na daraja lake la Elimu kwa kuzingatia sheria za nchi.
Dkt. msonde ameipongeza tume ya utumishi wa waalimu wilaya ya chamwino(TSC Chamwino) kwa kuanzisha bonanza la waalimu akisema kuwa jambo hilo linapaswa kuigwa na kila Halmashauri kwa ajili ya kuboresha ustawi wa waalimu. Pia ameitaka TSC chamwino kuendelea kushughulikia changamoto za waalimu mbali na shughuli yao mama ya kuratibu masuala ya kinidhamu bali kuwa kifua mbele katika kuwasaidia waalimu wanapokuwa na changamoto zinazowakabili. Alisema kuwa TSC inapaswa kuwa kimbilio kwa kila mwalimu.
“Tume ya utumishi la waalimu inawatumikia waalimu kwa kila kitu, Tsc ikiwa tulivu waalimu wanakuwa tulivu, TSC isipokuwa tulivu waalimu hawawezi kuwa tulivu, hivyo TSC inapaswa kuwa kimbilio la waalimu. Mwalimu akipata changamoto anapaswa kukimbilia kwenu TSC, customer care (huduma kwa mteja) hatakiwi kukwepa kero za wateja wake bali anatakiwa kuzichukua na kuzipeleka mahala sahihi, kama ni ya Mkurugenzi ipokee halafu ifikishe kisha mwelekeze mwalimu apate ufumbuzi usimfokee mwalimu hadharani.”
Katika hatua nyingine Dkt Msonde amewasihi walimu kuishi kwa upendo , umoja na mshikamano kwa malsahi mapana ya ustawi wa elimu ya wilaya ya chamwino kwa kuhakikisha kuwa wanafunzi wanapata elimu bora yenye ubora unaostahiki. Alisistiza suala la walimu kutokuogopa kupeleka changamoto zao TSC ili zipatiwe ufumbuzi kwa wakati kwa manufaa yao na Taifa kwa ujumla.
Awali akitoa taarifa fupi ya bonanza hilo , Katibu Msaidizi wa tume ya tumishi wa walimu Halmashauri ya wilaya ya Chamwino Paulina Kanumba alisema kuwa lengo la bonanza hilo ni kuwakutanisha waalimu pamoja, kuondoa dhana kwamba TSC ipo kwa ajili ya kuwaadhibu walimu kwa makosa ya kinidhamu pekee , na kufanya Tathmini ya pamoja ya mwisho wa mwaka kiutendaji na kuendeleza umoja na ushirikiano kwa walimu kupitia michezo.
Alisema kuwa bonanza hilo lililopewa jina la TSC bonanza 2023 limewakutanisha walimu katika michezo mbalimbali kama vile mpira wa miguu kwa wanaume, mpira wa pete(Netiboli), Riadha, kukimbia kwa gunia, kukimbia na yai mdomoni, na kukimbiza kuku ambapo washindi wa michezo hiyo walipewa zawadi za fedha Taslimu pamoja na vikombe.
Katika hatua nyingine ametoa shukrani za dhati kwa mgeni rasmi Dkt. Charles Msonde Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa kuweka kipaumbele katika utatuzi wa changamoto za walimu huku akimshukuru pia Rais wa Jamhuri ya muungano wa Tanzania Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kuwa msikivu katika kushughulikia maslahi ya walimu na namna anavyowathamini walimu.
“Nakushukuru sana Mheshimiwa mgeni rasmi kwa kuona umuhimu wa kuungana nasi leo, licha ya ratiba yako ngumu kwakuwa mimi ni shuhuda na sote tunajua kwamba wewe ni miongoni mwa watu wanaojitoa kutatua changamoto za waalimu, nitumie fursa hii pia kumshukuru Dkt. Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kumthamini mwalimu na kufanya shughuli mbalimbali za maendeleo nchini, tunashukuru sana”
Alisema mbali na shughuli za kimichezo bonanza hilo limehusisha ushiriki wa waalimu katika upandaji miti zaidi ya mia tano katika eneo la shule ya sekondari chamwino , kushiriki zoezi la uchangiaji damu salama na kupima virusi vya ukimwi bure kwa walimu walioshiriki bonanza hilo.
Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino
Sanduku la posta: 1126 Dodoma
Simu ya Mezani: 026 296 1511
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@chamwinodc.go.tz
Hakimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino. Haki zote Zimehifadhiwa.