Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Binilith S. Mahenge ameeleza kutokuridhishwa na idadi ya wakazi wa mkoa wa Dodoma waliojiunga kwenye Mfuko wa Afya ya Jamii CHF iliyoboreshwa. Mkuu wa Mkoa amesema hayo leo tarehe 6/7/2019 kwenye uzinduzi wa kampeni ya kuhamasisha wananchi kujiunga na bima ya afya ya CHF iliyoboreshwa ili waweze kupata matibabu kwa gharama nafuu ya shilingi 30,000 kwa mwaka mzima kwa kaya yenye watu sita, uzinduzi huo ulifanyika katika kijiji cha Nzali kata ya Chilonwa wilayani Chamwino.
"Hii asilimia 3% ya waliojiandikisha ni ndogo sana kwani ni sawa na wanachama 17,000 kati ya 460,000 wanaopaswa kuandikishwa mkoa wa Dodoma. Serikali ya awamu ya tano imewekeza sana katika sekta ya afya kuanzia miundombinu na dawa. Mfano hapa Dodoma zaidi ya vituo 22 vimejengwa, hospitali ya wilaya ya Chamwino na Hospitali kubwa ya Uhuru inayojengwa hapa papa Chamwino. Juhudi za Mheshimiwa Rais itakuwa bure kama wananchi hawatakuwa na bima, mara nyingi ni vigumu kumudu gharama za kulipia hapo hapo pindi wanapougua" Alisema Dkt. Mahenge
Aidha Mkuu wa Mkoa amewaagiza Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi mkoani Dodoma kuhakikisha wanaweka mkakati utakaowashirikisha viongozi wa ngazi zote za serikali ili kuwaelimisha na kuwahamasisha wananchi kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii ya CHF. Dkt. Mahenge amekabidhi kadi za CHF kwa wanachama 22 waliojiunga kwenye uzinduzi huo na amewashukuru wadau wakuu wa HPSS kwa ufadhili wanaoutoa katika shughuli za uendeshaji na uhamasishaji wa wananchi katika kujiandikisha na bima hiyo.
Nae Mbunge wa Chilonwa Mheshimiwa Joel Mwaka amemhakikishia Mkuu wa Mkoa kuwa yeye na wabunge wenzake wa Mkoa wa Dodoma watashiriki vyema kuhakikisha kampeni hii inafanikiwa.
Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino
Sanduku la posta: 1126 Dodoma
Simu ya Mezani: 026 296 1511
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@chamwinodc.go.tz
Hakimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino. Haki zote Zimehifadhiwa.