Kiongozi wa mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa mwaka 2023 ndugu Abdalla Shaibu Kaim ameipongeza Halmashauri ya wilaya ya Chamwino kwa kusimamia vizuri miradi ya maendeleo ambayo Mwenge wa Uhuru umefika na kujionea shughuli ambazo zimefanywa na kukuta zimekamilika kwa wakati.
Pongezi hizo amezitoa kwa mkuu wa wilaya ya Chamwino Mhe.Gifty Isaya Msuya pamoja na viongozi wote wa wilaya ya Chamwino kwa kushirikiana vizuri katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo iliyopo wilayani hapa.
Mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2023 umefanya ukaguzi wa nyaraka mbalimbali, kutembelea na kukagua miradi mbalimbali ya Maendeleo na kujionea juu ya ubora na viwango vilivyozingatiwa pamoja na kuangalia thamani ya matumizi ya fedha kama inaendana na maendeleo ya miradi iliyopo wilayani Chamwino.
Mwenge wa Uhuru ambao bado uko Mkoani Dodoma ulifika katika Wilaya ya Chamwino siku ya tarehe 04.10.2023 ambapo Mwenge huo wa Uhuru ulipokelewa kutoka wilaya ya Dodoma na makabidhiano hayo yalifanyika baina ya wakuu wa wilaya ya Dodoma Mhe. Jabir Shekimweri na Mhe. Gifty Isaya Msuya.
Baada ya kupokelewa kwa Mwenge huo ulitembelea Miradi mbalimbali ikiwemo Miradi ya Maji na Elimu, kutembelea na kujionea vijana wa kikundi cha ELLYDIZDON wanavyofanya kazi za uzalishaji na utengenezaji bidhaa mbalimbali pamoja na kutembelea shamba linalolimwa kwa kutumia kilimo cha kisasa la Mwekezaji wa kilimo David Mwaka ambalo lina ukubwa wa hekta 40 (Mtimbi Farm).
Mbali na Mwenge wa Uhuru kutembelea miradi hiyo ulipita katika Hospitali ya Uhuru iliyopo wilaya ya Chamwino na kutembelea mabanda mbalimbali yalyokuwa yakitoa Elimu za Lishe, Rushwa, Ukimwi, madawa ya kulevya na malaria.
Sanjari na hayo pia Mwenge wa Uhuru ulitembelea Mradi wa Uhifadhi wa Mazingira katika kitalu cha Miti Ikowa ambapo wakimbiza Mwenge Kitaifa na viongozi mbalimbali walipata fursa ya kupanda Miti katika Eneo Hilo.
Mwenge wa Uhuru umepitisha miradi yote ya Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino baada ya Miradi yote kukidhi vigezo vya ubora unaotakiwa.
Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino
Sanduku la posta: 1126 Dodoma
Simu ya Mezani: 026 296 1511
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@chamwinodc.go.tz
Hakimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino. Haki zote Zimehifadhiwa.