Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango ameweka jiwe la msingi kwenye kiwanda cha kusindika zabibu kilichopo Chinangali II Halmashauri ya wilaya ya Chamwino mkoani Dodoma. Uwekaji huo wa jiwe la msingi umefanyika wakati wa ziara ya siku nne ya kikazi atakayoifanya mkoani Dodoma iliyoanza leo Agosti 19 akitembelea na kukagua miradi ya maendeleo kwenye wilaya za mkoa wa Dodoma.
Akizungumza wakati wa ziara hiyo akiwa Wilayani Chamwino amepongeza jitihada za wakulima wa zabibu kwa kuzalisha zao hilo pamoja na kuwaomba kuongeza uzalishaji wa zao hilo kwani wanywaji mvinyo ni wengi na kuwepo kwa soko la uhakika kutakakotokana na uwekezaji wa kiwanda hicho.
Pia, ameitaka Wizara ya Kilimo kuhakikisha wanazalisha miche bora ya zao hilo la zabibu ili kuongeza thamani ya bidhaa hiyo sokoni kwani Tanzania hutumia bilioni 19.5 kwa mwaka kuagiza wastani wa lita milioni 10 za mchuzi wa zabibu kutoka nje ya nchi, hivyo uzalishaji bora wa zabibu na uwepo wa kiwanda hicho utaondoa changamoto ya zao hilo.
Kwa kulinda uzalishaji wa zao la zabibu Mh. Makamu wa Rais ameiagiza Wizara ya Kilimo kulinda na kutenga maeneo ya kilimo cha zabibu kutokana na ongezeko la kasi ya ujenzi katika mkoa wa Dodoma na kuwataka wananchi kutunza mazingira ya mkoa wa Dodoma kwa kutokukata miti hovyo ili kuepuka kutengeneza jangwa.
Aidha, amewahimiza wananchi na wadau kuchangamkia fursa za maendeleo zinazopatikana katika mkoa wa Dodoma ikiwemo kilimo cha zao la tende na komamanga kwani hustawi vizuri katika ardhi ya Dodoma pamoja na fursa za ufugaji wa samaki ili wananchi waweze kujikwamua kiuchumi na kuongeza pato la taifa.
Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino
Sanduku la posta: 1126 Dodoma
Simu ya Mezani: 026 296 1511
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@chamwinodc.go.tz
Hakimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino. Haki zote Zimehifadhiwa.