Leo Julai 30, 2019 Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan amekabidhi pikipiki 13 kwa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino na kuagiza zitumike kwenye shughuli zilizokusudiwa.
Pikipiki hizo zimetolewa na Wizara ya Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa kushirikiana na shirika la UN-Woman na zimekabidhiwa kwa Maafisa Maendeleo ya Jamii wa Kata 12 za Wilaya ya Chamwino ili ziwarahisishie kutekeleza majukumu yao pamoja na ufuatiliaji wa vitendo vya unyasaji wa wanawake na watoto. Pikipiki moja imekabidhiwa kwa Afisa Maendeleo ya Jamii ngazi ya Wilaya.
Makabidhiano hayo yamefanyika katika viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma wakati wa Uzinduzi wa Dawati la Kupambana na Unyanyasaji wa Wanawake na Watoto kwenye maeneo ya kufanyia biashara.
Makamu wa Rais ameeleza kuwa vitendo vya unyanyasaji wa Wanawake vimekuwa vikileta athari kubwa kiuchumi na kisaikolojia kwa jamii na amekemea tabia iliyozoeleka na baadhi watu kutoa lugha chafu na kuwatukana wanawake hadharani.
"Unakuta sokoni mtu mzima anaporomosha matusi ya nguoni kwa wanawake wajasiriamali na wengine hudiriki mpaka kuwashika maungo yao na pengine mbele ya watoto wao. Huu ni unyanyasaji ambao sitakubaliana nao, ndio maana tumezindua Dawati hili". Alisema Makamu wa Rais.
Kwa upande wake Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mh. Ummy Mwalimu amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri nchini kuhakisha wanatoa mikopo mikubwa yenye tija kwa wanawake na ameonya Madiwani kutotumia mikopo hiyo kisiasa.
Aidha Makamu wa Rais Mh. Samia ametembelea Soko la Majengo lililopo jijini Dodoma na kufanya uzinduzi wa Dawati la Kupinga Unyanyasaji wa Wanawake na Watoto ambalo limezinduliwa rasmi katika Wilaya za Dodoma na Shinyanga.
Makamo wa Rais akiwa kwenye picha ya pamoja na viongozi wa Wilaya ya Chamwino baada ya kukabidhi pikipiki
Baadhi ya Maafisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino waliokabidhiwa pikipiki
Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino
Sanduku la posta: 1126 Dodoma
Simu ya Mezani: 026 296 1511
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@chamwinodc.go.tz
Hakimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino. Haki zote Zimehifadhiwa.