Katibu Tawala wa mkoa wa Dodoma Ndg: Kaspar Kaspar Mmuya amefanya ziara ya kikazi Wilayani Chamwino Mei 30,2024 kwa lengo la kukagua miradi ya maendeleo pamoja na kuongea na watumishi.
Akizungumza katika kikao kazi hicho amewapongeza kwa utendaji mzuri na kuwaelekeza kuwa waendelee kufanya kazi kwa tija na kwa kufuata sheria kanuni, taratibu, miongozo na maelekezo ya viongozi, pamoja na mila na desturi ya eneo wanalofanyia kazi.
"Nawapongeza kwa sababu mnafanya kazi kwa upendo na kwa kujitoa kwa niaba ya Mheshimiwa Rais." Alisema.
Katika kutekekeza wajibu amewataka watumishi kujua wajibu wao unaoendana na vyeo vyao.
Vilevile amewaelekeza watumishi kutumia busara chanya yenye matokeo makubwa zaidi pale inapohitajika katika kutekeleza majukumu yao kwa manufaa ya Umma na Taifa.
Amewataka watumishi kutoa huduma kwa haki na kusisitiza kuwa hapendi huduma inunuliwe. "Toeni huduma kwa kufuata haki na usawa." Alisema Katibu Tawala.
Katibu Tawala Mkoa amezungumzia pia suala la ukusanyaji wa mapato ya Halmashauri ambapo amesema mapato yanapaswa kukusanywa vizuri na kurudisha kile kilichokusanywa kwa wananchi kwa kuwapelekea maendeleo.
" Mheshimiwa Rais anapotembea kwenye ziara zake anaangalia mbona ile hela ninayoambiwa na Kamishina wa kodi Alfayo Kidata haioni kwenye maisha ya watanzania? Alisema Katibu Tawala.
Vilevile amewaasa watumishi kuhusu kuongeza kipato na uchumi wa familia na kuwasisitiza kupanda miti ya matunda kwenye makazi yao hata kwa wale wanaoishi kwenye nyumba za kupanga kwani kufanya hivyo hakutawaathiri chochote. Alitolea mfano mti mmoja wa parachichi unauwezo wa kukuzalishia mavuno ya wastani wa laki tatu kwa mwaka.
Amewaasa pia watumishi kupendana wanapokuwa kazini na wasipende kuwa na tabia za chuki na kupenda wenzao waharibikiwe. Ameeleza kuwa kuna watu furaha yao huwa ni kuona wenzao wanaharibikiwa.
"Muda mwingi tunautumia tukiwa kazini, ndugu yako mama yako, baba yako, rafiki yako ni watu hawa ambao wamekuzunguka. Inaniuma mno kuwa mimi bosi wangu simpendi au msaidizi wangu simpendi, au mtumishi wa chumba jirani simpendi. Kwa sababu ukichukia kuna seli fulani za mwili wako zinavunjika." Alisema.
"Unapoishi kwa upendo na mwenzako unamuongezea ari ya kufanya kazi na kwa kufanya hivyo tija inaongezeka. Watu wakiamka asubuhi wapende kwenda kazini." Alisema.
Watumishi pia wamekumbushwa wajibu wa kusikiliza kero za wanaanchi na kuzipatia ufumbuzi kama kaulimbiu ya mkoa inavyojielekeza inayosema "KERO YAKO WAJIBU WANGU"
Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino
Sanduku la posta: 1126 Dodoma
Simu ya Mezani: 026 296 1511
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@chamwinodc.go.tz
Hakimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino. Haki zote Zimehifadhiwa.