Waheshimiwa Madiwani wamepatiwa elimu kuhusu ugonjwa wa mlipuko wa homa ya MPOX ambayo tayari imeshazikumba baadhi ya nchi za Afrika Mashariki kama vile Kenya na Burundi kwenye Mkutano wa Baraza la Madiwani robo ya nne ya mwaka wa fedha 2023/2024 uliofanyka ukumbi wa mikutano wa Halmashauri Agosti 27, 2024.
Akizungumza kwenye kikao hicho Dkt. Sophia M. Nchimbi mratibu wa tiba, dharura pamoja na maboresho Halmashauri ya Chamwino amesema ugonjwa huo unatokana na virus vya monkeypox ambavyo vinapatikana kwenye wanyama jamii ya nyani na wanyama wengine kama paka na panya.
Daktari alieleza njia zinazotumika kuambukiza ugonjwa huo ikiwemo kula kitoweo ambacho hakijaaiva vizuri chenye kutokana na nyama pori jamii hiyoau kugusana nao au kushika kinyesi chao, kushika majimaji au kushikana na mgonjwa, nguo, vyombo na vitu vingine vilivyotumika na mgonjwa wa Mpoxi pamoja na kujamiiana na mtu mwenye ugonjwa huo, kubusiana.
Dalili za ugonjwa imeelezwa kuwa ni kutoka malengelenge au vipele kama tetekuwanga, uchovu wa mwili, maumivu ya mgongo, maumivu ya misuli, kuvimba mitoki ya mwili, vidonda vya koo, maumivu ya kichwa pamoja na homa.
Amewataka Wahe. Madiwani wasaidie kuwaelimisha wananchi kuhusu ugonjwa huu jinsi unavyoambukiza pamoja na jinsi ya kujikinga ambapo ameeleza kuwa wananchi wanapaswa kunawa mikono vizuri kwa kutumia sabuni na maji tiririka pamoja na vitakasa mikono. Vilevile kuepuka vitu vinavyoweza kusababisha maambukizi.
Aidha Daktari ameelekeza waweze kutoa taarifa pindi wanapoona mtu mwenye dariri za ugonjwa na pia awahishwe sehemu ya kutolea huduma za afya.
Vilevile Serikali Wilayani Chamwino imeahidi kutoa mbegu za ruzuku kwa wakulima kwa msimu wa kilimo wa 2024/2025 mapema mwanzoni mwa msimu pamoja mbolea ya ruzuku.
Hayo yameelezwa na mkuu wa Idara ya Kilimo na mifugo wa Wilaya Ndg: Godfrey Mnyamale alipokuwa akijibu swali la Mhe. Diwani wa Majeleko Musa Omary aliloliuliza kwenye mkutano wa Baraza la Madiwani akihofia mbegu kuchelewa kutolewa kwa mbegu kunakoweza kupelekea wakulima kuchelewa kupanda na hivyo kupata mavuno hafifu.
Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino
Sanduku la posta: 1126 Dodoma
Simu ya Mezani: 026 296 1511
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@chamwinodc.go.tz
Hakimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino. Haki zote Zimehifadhiwa.