Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mheshimiwa Anthony Mtaka amewataka viongozi wa Serikali na watumishi wa Wilaya ya Chamwino kulipa kipaumbele suala la elimu ambalo ndilo litakaloweza kuwaletea maendeleo na kuinua hali ya uchumi wao.
Hayo ameyasema kwenye kikao kazi kilichofanyika kwenye eneo la ofisi za Halmashauri jana mei 12, 2022. "Sitakuwa na mchezo kwenye suala la elimu. Kila sehemu yenye elimu nzuri na uchumi pia huwa mzuri."Alisema Mkuu wa Mkoa.
Aidha aliwapongeza viongozi wa Serikali za vijiji na walimu waliofanya vizuri kwenye maeneo yao na aliahidi kufanya mikutano kwenye maeneo hayo ili kuweka hamasa zaidi katika kuinua ufaulu wa wanafunzi.Mhe. Mkuu wa mkoa aliahidi kutoa zawadi ya shilingi 50,000/= kwa kila mwalimu kwa walimu wote sita wa shule ya msingi Loje waliolima alizeti mwaka uliopita wa 2021 na kufanikiwa kupata pesa zilizowawezesha kununua mashine ya kudurufu mitihani ya shule hiyo.
Akiunga mkono juhudi hizo Mhe. Mkuu wa Wilaya ya Chamwino Bibi Gift Msuya aliahidi kutoa shilingi 300,000/= kutoka kwenye fedha za kampeni yake ya Nishike Mkono Kuinua Elimu Chamwino.
Vilevile Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma bibi Fatuma Mganga ameelekeza kuwa ili kuboresha hali ya ufaulu kwa wanafunzi nafasi za uongozi zisiwe za kudumu, mwalimu Mkuu anayefanya vibaya aondolewe na ateuliwe mwingine kushika nafasi yake.
" Mbinu hii ya kuwaondoa walimu wakuu waliofanya vibaya na kuteuawa wengine niliitumia nilipokuwa Bahi na nilifaulu, Bahi ikawa ya kwanza Kimkoa.' Alisema Katibu Tawala.
Pia aliwaelekeza walimu kuwashawishi wanafunzi kusoma masomo ya sayansi ili kupata madaktari na manesi. Alieleza kuwa watoto wasipofaulu wazazi hawawezi kuwa na moyo wa kuchangia."Mzazi anasomesha mtoto anapata daraja la nne na sifuri, pasipo kuona watoto wanafaulu hawezi kuhamasika kuchangia."Alisema Katibu Tawala.
Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino
Sanduku la posta: 1126 Dodoma
Simu ya Mezani: 026 296 1511
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@chamwinodc.go.tz
Hakimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino. Haki zote Zimehifadhiwa.