Chamwino Yanyakua vikombe Vitatu Mashindano ya UMISSETA
Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino imejinyakulia vikombe vitatu baada ya kushika nafasi ya kwanza katika mashindano ya UMISSETA ngazi ya Mkoa.
Vikombe hivyo vimekabidhiwa kwa Mkurugenzi Mtendaji Wilaya Ndugu Athumani H. Masasi na Afisa Elimu Sekondari Ndugu David Mwamalasi Ofisini kwake mapema wiki ambapo nae alivikabidhi kwa Mwenyekiti wa Halmashauri Ndugu Samwel A. Kaweya.
Akizungumza katika hafla fupi ya kukabidhi vikombe hivyo Afisa Elimu Sekondari alisema, “Chamwino imeshinda nafasi ya kwanza katika michezo ya mpira wa pete (netball), mpira wa wavu(volleyball) wasichana na sanaa za maonyesho (ngoma).”
Aliendelea kueleza kuwa Wilaya pia imefanikiwa kupata ushindi wa pili kwa michezo ya mpira wa miguu (football), mpira wa kikapu(basketball) na mpira wa wavu ( volleyball) wavulana ambapo walizawadiwa vyeti kwa kushika nafasi hiyo ya pili.
Vilevile alieleza kuwa Wilaya imefanikiwa kushinda mchezo wa Riadha mita 100 na 800 Wavulana.
Aidha katika taarifa yake alisema kuwa Wilaya imefanikiwa kupeleka uwakilishi wa wanamichezo ishirini na tano (25) kati ya mia moja (100) waliochaguliwa kuuwakilisha Mkoa ngazi ya Taifa.
Kati yao riadha wavulana wawili, mpira wa miguu wavulana wawili, mpira wa pete wasichana wanne (4), mpira wa kikapu wavulana wawili (2) na mpira wa wavu wavulana mmoja (1) na kikundi cha ngoma jumla ya waimbaji 14.
Ushindi huo umepokelewa kwa furaha kubwa na viongozi wote. Wakiongea kwa nyakati tofauti Mwenyekiti wa Halmashauri pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wamewataka Wataalam kuhakikisha wanafanya vizuri kwenye Nyanja zote na si kwenye michezo tu.
Mkurugenzi Mtendaji Wilaya pia alitimiza ahadi yake aliyoitoa kwa wanamichezo ya kutoa shilingi 200,000/= kwa kila kikombe watakachokipata katika mashindano hayo ya ngazi ya Mkoa kama motisha kwa wanamichezo hao.
Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino
Sanduku la posta: 1126 Dodoma
Simu ya Mezani: 026 296 1511
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@chamwinodc.go.tz
Hakimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino. Haki zote Zimehifadhiwa.