Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino Mkoani Dodoma leo Januari 12, 2021 imeadhimisha siku ya Mapinduzi ya Zanzibar kwa kupanda Miti katika eneo la pembezoni mwa Hospitali ya Uhuru Wilayani humo ambapo zaidi ya miche 2000 ya miti imepandwa.
Katika Zoezi hilo lililoongozwa na Mkuu wa mkoa wa Dodoma Mheshimiwa Bilinith Mahenge ameambatana na viongozi mbalimbali Serikali akiwepo Katibu Tawala wa Mkoa pamoja na viongozi wengine kutoka Ofisi ya Mkoa na Jiji la Dodoma, Mkuu wa Wilaya, Katibu Tawala wa Wilaya, Mheshimiwa Mwenyekiti na Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri, Mkurugenzi na Wakuu wa Idara na Taasis mbalimbali Wilayani Chamwino na wanafunzi wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM) kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM).
Akizungumza baada ya zoezi la upandaji miti aliwashukuru wote kwa kazi nzuri waliyoifanya na hususani kwa wanafunzi wa UDOM waliofika Ofisini kwake na kuomba kupanda miti eneo la Hospitali ya Uhuru ikiwa ni kuunga Mkono juhudi za Mheshimiwa Rais ambapo amewekeza fedha nyingi katika ujenzi wa Hospitali hiyo.
Aliwaomba wanafunzi wafikishe salamu zake kwa Mkuu wa Chuo kwa kuwaruhusu kushiriki katika zoezi hilo.
Mkuu wa Mkoa ameomba zoezi hilo liwe endelevu na lisisubiri tu siku za sherehe. ‘‘Naomba zoezi hili liwe endelevu na si kusubiri siku za sherehe peke yake,’’ amesema Mkuu wa Mkoa.
Aliongeza kuwa tunao wajibu mkubwa wa kupanda na kuitunza miti hii, ili kuweza kukabiliana na mabadiliko ya tabia ya nchi yanayosababishwa na hewa ukaa inayozalishwa kutokana na viwanda pamoja na shughuli nyingine za kibinadamu.
‘‘shughuli za kibinadamu zinapoongezeka zinaleta mabadiliko ya tabia ya nchi,hivyo ni lazima tuyatunze mazingira yetu na kukabiliana na mabadiliko ya hali ya hewa kwa kupanda miti’’ amesema Mkuu wa Mkoa.
Aidha aliongeza kuwa watazidi kuwaomba wanafunzi wa UDOM wasaidie kupanda miti kwenye maeneo mengine watakayoyapanga. Aliomba tupande miti tuwaandalie vizazi vijavyo mazingira mazuri kama sisi tulivyoikuta misitu iliyopandwa na mababu zetu.
Baada ya zoezi la upandaji miti wanafunzi wa UDOM walikwenda kujitolea Damu katika Hospitali ya Uhuru kwa ajili ya kusaidia wagonjwa watakaokuwa na uhitaji wa kuongezewa damu.
Wanafunzi wa UDOM wakijitolea damu katika Hospitali ya Uhuru Wilayani Chamwino.
Na ofisi ya TEHAMA - Chamwino
Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino
Sanduku la posta: 1126 Dodoma
Simu ya Mezani: 026 296 1511
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@chamwinodc.go.tz
Hakimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino. Haki zote Zimehifadhiwa.