Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino imeadhimisha kilele cha siku 16 za kupinga ukatili zilizoanza kuanzia tarehe 25 Novemba na kuhitimishwa 10 Desemba, 2024. Maadhimisho hayo yalifanyika katika kata ya Huzi.
Kilele cha Maadhimisho hayo yaliyobeba kauli mbiu “Kuelekea Miaka +30 ya Beijing Chagua Kutokomeza Ukatili wa Kijinsia” yaliadhimishwa mbele ya mgeni rasmi Mkuu wa Wilaya ya Chamwino Mh. Janeth Mayanja.
Akizungumza katika kilele cha maadhimisho hayo Mh. Janeth Mayanja amewahasa Wananchi waliojitokeza katika maadhimisho hayo kutoa haki sawa kwa watoto wote wa kiume na wa kike na kuhakikisha watoto wa kike wanapatiwa mahitaji yao ya msingi sawa na watoto wa kiume.
Aidha, amekumbusha pia wakati harakati za kutetea haki za mtoto wa kike zinaendelea watoto wa kiume nao wasiachwe nyuma na wapatiwe mahitaji yao ya msingi bila kubaguliwa.
Sanjari na hilo, Mh. Mayanja amewataka Wananchi kuachana na mila na desturi zinazokandamiza jinsia moja ikiwemo kuozeshwa kwa watoto wa kike katika umri mdogo unaopelekea kukosa haki zao za msingi kama elimu, na kusisitiza pia mwanamke na mwanaume wana haki sawa.
Aidha, DC Mayanja amehaidi kuwachukulia hatu wazazi na familia ambazo wanatatua mambo ya ukatili wa kijinsia ikiwemo ubakaji na ulawiti nyumbani bila kufikisha kesi hizo katika vyombo vya sheria.
Kwa upande wa Afisa Maendeleo ya Jamii Wilaya ya Chamwino Bi. Zaina Msangi ameelezea lengo la kuadhimisha siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia, ikiwa ni kuunganisha nguvu kati ya Serikali na Taasisi zake pamoja na wadau wa maendeleo kupaza sauti kwa ajili ya kuwasemea wale wanaofanyiwa ukatili wakiwemo wanawake na watoto.
Maadhimisho hayo ya siku 16 za kupinga ukatili yalipambwa pia na burudani kutoka vikundi mbalimbali vilivyosherehesha tukio hilo, pamoja na wadau na mashirika yasiyo ya Kiserikali ikiwemo World Vision, Epic na Tanzania Women Chamber of Commerce (TWCC) waliochangia kutoa mada na kufanikisha kilele hicho.
Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino
Sanduku la posta: 1126 Dodoma
Simu ya Mezani: 026 296 1511
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@chamwinodc.go.tz
Hakimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino. Haki zote Zimehifadhiwa.