Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa amewasilisha makadirio ya Bajeti ya Ofisi ya Rais TAMISEMI kwa mwaka wa Fedha 2017/2018 Bungeni mjini Dodoma.
Akiwasilisha makadirio ya Ofisi ya Rais TAMISEMI, Mhe. Simbachawene amesema jumla ya shilingi 6,023,559,414,000 zitatumika katika mwaka 2017/18 ambapo itahusisha mishahara, matumizi ya kawaida na utekelezaji wa iradi ya Maendeleo kwa Ofisi ya Rais TAMISEMI, Tume ya Utumishi wa Walimu, Mikoa na Halmashauri.
Kuhusu mafanikio ya TAMISEMI, amesema hadi kufikia Machi, 2017 jumla ya Halmashauri 177 kati ya 185 sawa na asilimia 96.2 zinatumia mfumo wa kielektroniki ambao umeboresha ufanisi katika ukusanyaji wa mapato.
Pia migogoro ya ardhi katika Mamlaka za Serikali za Mitaa imeundiwa timu ya wataalamu inayoshirikisha Wizara ya Ardhi, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Maliasili na Utalii, Wizara ya Kilimo na Wizara ya Maji ili kupata njia bora ya kumaliza migogoro.
Kwa upande wa wafanyakazi hewa amesema, “jumla ya watumishi 13,369 ambao ni watoro, wastaafu na waliofariki wameondolewa katika orodha ya malipo ya mishahara ya Serikali”, ambapo watumishi 541 walikuwa wa Sekretarieti za Mikoa na watumishi 12,828 wametoka katika Mamlaka za Serikali za Mitaa. Aidha, shilingi bilioni 2.7 zimerejeshwa Serikalini na pia waliohusika na upotevu huo wamechukuliwa hatua.
Pia, Ofisi ya Rais TAMISEMI imekamilisha ufungaji wa Tovuti katika Mikoa 26 na Halmashauri 185 ili kuwawezesha Wadau mbalimbali kupata taarifa na kufahamu majukumu yanayotekelezwa katika Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa, sambamba na hilo mafunzo ya tovuti yametolewa kwa Maafisa habari na TEHAMA wa Mikoa na Halmashauri zote juu ya matumizi yaliyokusudiwa ili kuhabarisha Watanzania masuala yanayotekelezwa na Serikali pamoja na kuimarisha Utawala Bora.
Katika mwaka 2017 katika shule za msingi wanafunzi wapatao 3,188,149 wameandikishwa kuanza darasa la Awali na Darasa la Kwanza sawa na ongezeko la wanafunzi 319,849 ikiwa ni matokeo ya Mpango wa Serikali wa utoaji wa Elimumsingi bila malipo unaotoa fursa kwa watoto wengi kupata elimu.
Aidha, Serikali imelipa madeni ya walimu yasiyo ya Mishahara kiasi cha shilingi bilioni 10.05, ununuzi wa vifaa vya Elimu Maalum shilingi bilioni 4.2, ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya Shule za Msingi 19 kwa shilingi bilioni 1.75.
Mhe. Simbachawene amesema, Halmashauri 184 zimetenga shilingi bilioni 56.8 kutokana na mapato ya ndani kwa ajili ya Mfuko wa Vijana na Wanawake. Fedha hizo zimetumika kwa ajili ya mikopo kwa vikundi vya ujasiriamali vya Vijana na Wanawake ili kukuza kipato na ajira.
Amesema kuwa katika mwaka huu wa fedha, Ofisi ya Rais - TAMISEMI, Taasisi zilizo chini yake, Mikoa na Mamlaka za Serikali za Mitaa zinatarajia kukusanya shilingi 713,187,789,615 zitakazotokana na mauzo ya vifaa chakavu na nyaraka za zabuni, faini mbalimbali, marejesho ya masurufu na mishahara, ikiwemo kodi na ushuru kwa upande wa Mamlaka za Serikali za Mitaa kulingana na Sheria ya Fedha za Serikali za Mitaa
Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino
Sanduku la posta: 1126 Dodoma
Simu ya Mezani: 026 296 1511
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@chamwinodc.go.tz
Hakimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino. Haki zote Zimehifadhiwa.