Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino leo tarehe 27 Januari, 2025 imesheherekea siku ya kuzaliwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kwa kupanda miti katika shule ya Mkoa ya Wasichana Manchali.
Zoezi hilo limeongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Chamwino Mh. Janeth Mayanja ambaye aliongozana na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri Ndg. Godfrey Mnyamale pamoja na Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya kupanda miti 600 ya matunda na kivuli.
Akizungumza baada ya zoezi hilo la upandaji wa miti mh. Mayanja amemuelekeza mkuu wa shule ya wasichana Manchali kuitunza miti hiyo.
“Naelekeza miti hii itunzwe, kama mnavyojua shule hii bado ipo wazi sana ukilinganisha na maeneo mengine, Mkuu wa shule wanafunzi muwafundishe elimu ya kujitegemea ikiwemo kutunza miti hii ambayo badae itakuja kuwasaidia” alisema Mh. Mayanja.
Sanjari na hilo, Mhe. Mayanja amewaagiza Wakala wa Misitu (TFS) Wilaya ya Chamwino kupeleka miti katika ofisi za vijiji vyote 107 ili wananchi wapate fursa ya kuchukua miti hiyo kwa ajili ya kupanda katika makazi yao.
Aidha, zoezi hilo la upandaji wa miti lilitamatishwa na ukataji wa keki pamoja na nyimbo za kumtakia heri ya siku ya kuzaliwa Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino
Sanduku la posta: 1126 Dodoma
Simu ya Mezani: 026 296 1511
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@chamwinodc.go.tz
Hakimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino. Haki zote Zimehifadhiwa.