Mheshimiwa Ikupa Achangia Fedha Kituo cha Wasiioona Buigiri
Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu mwenye dhamana ya walemavu Mheshimiwa Stella Alex Ikupa amewachangia fedha walemavu wasiioona wanaoishi katika kituo cha Matembe bora kilichopo katika kijiji cha Buigiri Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino.
Mchango huo ameutoa jana alipofanya ziara kituoni hapo baada ya kupokea changamoto mbalimbali kutoka kwa walemavu hao.
Mhe. Stella A. Ikupa amewapatia kiasi cha shilingi 300,000/= ambapo pia aliungwa mkono na wabunge Joel Mwaka wa jimbo la Chilonwa na Fatuma M. Toufiq Mbunge Vitimaalum Mkoa wa Dodoma ambao wametoa shilingi 150,000/= kwa kila mmoja na hivyo kufanya jumla ya mchango wote kuwa shilingi 600,000/=
Amewaeleza kuwa kupitia fedha hiyo wataamua wao wenyewe waanze kutatua changamoto ipi kati ya walizoziwasilisha kwake.
Kuhusu changamoto ya tanki la maji pamoja na hati miliki ya kituo hicho Mkurugenzi Mtendaji Ndugu Athumani H. Masasi ameahidi kuzifanyia kazi kwa kutenga fedha kwenye bajeti ya mwaka 2019/2020 kwa ajili ya tanki la maji na kuhakikisha hati miliki inapatikana kwa kuwa yote yako ndani ya uwezo wa Halmashauri.
Kuhusu changamoto ya suala la walemavu kupatiwa viwanja kwa ajili ya makazi Mhe. Naibu Waziri Ikupa ameielekeza Halmashauri kuwa pindi inapouza viwanja watu wenye ulemavu wapewe kipaumbele na wapewe muda mrefu kidogo wa kulipia.
Aidha Mhe. Naibu Waziri ametoa maagizo mbalimbali ikiwemo suala la kutenga bajeti kwa ajili ya kununua mafuta ya watu wenye ulemavu wa ngozi, kutenga maeneo ya biashara kwa ajili ya watu wenye ulemavu na kukamilisha zoezi la uundaji wa kamati za walemavu kwa vijiji ambavyo havijaunda.
Vilevile ameielekeza Halmashauri kuhakikisha inakutana na watu wenye ulemavu na kuwauliza mahitaji yao na kuyatengea fedha katika bajeti ya mwaka wa fedha 2019/2020.
Mhe. Naibu Waziri Ikupa ameipongeza Halmashauri kwa namna inavyoshughulikia masuala ya walemavu ikiwemo suala la kutoa mikopo ya 2% pamoja na kuwa na dirisha la kuwahudumia walemavu wanapokwenda kupata matibabu.
Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino
Sanduku la posta: 1126 Dodoma
Simu ya Mezani: 026 296 1511
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@chamwinodc.go.tz
Hakimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino. Haki zote Zimehifadhiwa.