" Nimeridhishwa na mradi unavyoendelea, kazi iliyofanyika ni nzuri".
Maneno haya yamesemwa na Waziri wa Kilimo Mhe. Hussen Bashe alipofanya ziara ya kukagua utekelezaji wa miradi ya kilimo Wilayani Chamwino Septemba 28, 2022.
Miradi iliyokaguliwa ni mradi wa kilimo cha zabibu Chinangali na mradi wa ujenzi wa Bwawa la umwagiliaji Membe.
Katika miradi yote miwili Mhe. Bashe ameridhishwa na kazi inavyoendelea na ametoa maelekezo mbalimbali kwa wasimamizi wa miradi hiyo.
Kwenye mradi wa shamba la zabibu Chinangali wenye ekari 600, ameelekeza wakulima waliopo kwenye eneo lililobaki jirani na shamba hilo waorodheshwe na maeneo yao yaingie kwenye mradi huu ili wapate walau ekari 1000 kwa ajili ya kilimo cha mashamba makubwa( block farming).
Mhe. Waziri pia ameeleza adhima ya Serikali ya kujenga kiwanda cha kuchakata na kutengeneza mchuzi wa zabibu ambapo wakulima wataongeza thamani ya zao hilo nakuuza kwa bei nzuri kuliko wanavyouza sasa ikiwa ni pamoja na kuwa na soko la uhakika.
' Tukifanikiwa kujenga kiwanda maana yake wakulima watauza mchuzi wa zabibu. Kilo moja ya zabibu kwa sasa ni shilingi elfu moja lakini lita moja ya mchuzi wa zabibu ni shilingi elfu tatu, hivyo mkulima ataondokana na adha ya kukosa soko. Halmashauri pia itaweza kupata ushuru mzuri ( produce cess). Alisema Mhe. Waziri.
Naye Mwenyekiti wa chama cha ushirika cha CHABUMA AMCOS ndugu David Mwaka ameeleza kuwa kazi ya kusafisha shamba inaendelea vizuri, tayari wamesafisha kwa 99% na kazi ya kusambaza drippers inaendelea. Amemuomba Mhe. Waziri wazo lake la kujenga kiwanda alifanyie kazi kunusuru soko la zabibu.
" Mwaka huu zabibu nyingi zimeharibikia shambani tunakuomba lile wazo lako la kujenga kiwanda ulifanyie kazi kunusuru soko la zao la zabibu". Alisema Mwenyekiti wa CHABUMA AMCOS.
Akiwa kwenye mradi wa ujenzi wa bwawa Membe, Mhe. Waziri amempongeza Mkandarasi kwa kazi nzuri.
Vilevile Mhe. Bashe ametoa maagizo kwa Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri kupitia upya na kuorodhesha wakulima wanaolima kwenye eneo la mradi wa Membe ili wapewe maeneo na eneo linalobaki litagawiwa kwa vijana.
"Naagiza Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi Mtendaji mfanye upya mapitio ya wakulima wanaolima kwenye eneo la mradi ili tuwatambue na kuwagawia maeneo kama ni ekari 5 au 10 ili asije kuibuka mtu na kusema eneo lake limechukuliwa, na kisha eneo linalobaki tutaligawa 9kwa vijana. Tunataka kilimo chenye tija na kuondokana na ukulima mdogomdogo wa kujikimu". Alisema Mhe. Bashe.
Vilevile Mhe. Waziri ameelekeza Mkurugenzi Mtendaji wa Wilaya kukaa na vyama vya ushirika na kufanya tathimini ya mavuno kwa wakulima wadogo waliokopeshwa fedha na benki ya CRDB ili kuona ni kiasi gani kinaweza kulipika na kwa wale ambao hawakuwa na mavuno mazuri waorodheshwe walipe kwa msimu ujao wa 2022/2023.
Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino
Sanduku la posta: 1126 Dodoma
Simu ya Mezani: 026 296 1511
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@chamwinodc.go.tz
Hakimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino. Haki zote Zimehifadhiwa.