Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Rosemary Senyamule amewahimiza wananchi kuweka mkakati wa kufanya mazoezi kwa lengo la kuweka sawa miili yao ili kukabiliana na magonjwa ambayo yamekuwa yakiwa kumba mara kwa mara.
Mhe. Senyamule ameyasema hayo leo Wilayani Chamwino kwenye mkutano wa kwanza wa sayansi za afya uliondaliwa na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kwa lengo la kuhakikisha afya bora kwa wote.
"Lakini wapo ambao hata hayo mazoezi ya kutembea hawafanyi kwahiyo niendelee kutoa shime suala la mazoezi liwekewe mkakati nakumbuka tuliwahi kukaa kwenye kikao tukaazimia maafisa ustawi wa Jamii kwenye kila kata watafute eneo wawawekee wazee walau mara moja kwa wiki kuwakutanisha ili wafanye mazoezi yanayoendana na umri wao",amesema.
Pia amewaomba wananchi kuendelea kuhamasishana ili wajitokeze kwenda kupima Afya zao na kujua mapema juu ya kile kinachowatatiza kabla ya ugonjwa haujawa mkubwa na kuweza kutibiwa mapema.
Aidha, ameongeza kuwa elimu ya afya inapaswa kuendelea kutiliwa makazo kwani ni nyenzo muhimu katika kupambana na magonjwa yasiyo ambukiza na kuimarisha ustadi wa kimaisha huku akiongeza kuwa wananchi hawana budi kuzingatia ulaji ulio bora.
"Elimu ya Afya ni nyenzo muhimu katika mapambano dhidi ya Magonjwa yasiyoambukiza, elimu ya mabadiliko ya mtindo wa maisha hususani ulaji unaofaa, umuhimu wa mazoezi na aina zake, madhara ya utumiaji wa tumbaku na mazao yake, unywaji hatarishi wa pombe na njia zake na kuepukana na msongo wa mawazo unaosababisha magonjwa yasiyo ambukiza yatafundishwa na wataalam waliobobea katika maswala haya", ameongeza.
Akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa chuo Kikuu cha Dodoma Prof. Albino Tenge amesema kuwa moja kati ya lengo kuu la mkutano huo ni kutimiza lengo la tatu la maendeleo endelevu la umoja wa mataifa linalolenga maisha yenye afya bora na ustawi kwa watu wote.
"Tuna ushahidi wa kutosha kwamba magonjwa yasiyo ambukizwa kama vile moyo, kisukari, shinikizo la damu la juu na magonjwa mengine yameongezeka duniani kote na athari zake wote tunaziona na zimekuwa kubwa zaidi hasa katika nchi za kipato cha chini na kati",amesema.
Ameongeza kuwa katika zoezi hilo wanategemea kuwafikia watanzania 1000 mpaka 1793 lengo likiwa ni kuongeza ufahamu kwa wananchi kuhusu magonjwa ya kuambukiza na yasiyoambukiza
Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kwa kushirikiana na Ofisi ya mkuu wa mkoa wa Dodoma kimendaa siku mbili za Uchunguzi wa kibingwa Bure unaofanyika katika Hospitali ya Uhuru iliyopo wilayani Chamwino mkoani Dodoma.
Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino
Sanduku la posta: 1126 Dodoma
Simu ya Mezani: 026 296 1511
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@chamwinodc.go.tz
Hakimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino. Haki zote Zimehifadhiwa.