Tume ya Watumishi wa Walimu (TSC) Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino leo tarehe 27 Machi, 2025 wametoa tuzo kwa Walimu wa shule za Sekondari na Msingi waliofanya vizuri kwa kuleta ufaulu katika mitihani ya kitaifa ya darasa la saba, kidato cha pili, kidato cha nne na sita ya mwaka 2024, tuzo hizo zilitolewa katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri.
Utolewaji wa tuzo hizo ni sehemu ya kuongeza hamasa inayotolewa na TSC Wilaya ya Chamwino kwa Walimu kwa kutambua mchango na jitihada zao katika kuongeza ufaulu wa Wanafunzi.
Akizungumza katika hafla hiyo ya utolewaji wa tuzo mgeni rasmi Ndg. Romuli John ambaye alimuwakilisha Katibu wa Tume ya Utumishi wa Walimu Taifa amempongeza Katibu wa TSC Wilaya Chamwino Bi. Paulina Kanumba pamoja na timu anayofanyanayo kazi kwa ubunifu wa kuandaa tuzo na ushirikiano walionao.
“Pamoja na pongezi hizi kwa Katibu nipongeze timu anayofanyanayo kazi pale TSC nina uhakika ushirikiano wenu, maelewano yenu na mshikamano ndo umewafikisha hapa vinginevyo basi ofisi ingekuwa haiendi, nimesikia tangia tunakuja ofisi ya TSC ukiwa unakuja sasa mtu anaweza kupiga hata stori”. Alipongeza Ndg. Romuli.
Aidha, Ndg. Romuli amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa mchango wake mkubwa kuinua sekta ya elimu nchini kwa kuelekeza fedha nyingi kwenye sekta hiyo.
Sambamba na pongezi hizo amewapongeza pia walimu pamoja na kuwaomba kuhakikisha wanasimamia suala la maadili bora kwa Wanafunzi na katika utendaji wa majukumu yao.
“Tunatakiwa tupambane kuhakikisha maadili yanakolea tusiliache hilo nyuma kwahiyo niombe walimu tuliopo hapa kama wawakilishi wa wengine twendeni tukaeneze hii kwamba upande wa maadili tuweke mfumo imara sana”. Alisema Ndg. Romuli.
Kwa upande wa Katibu wa TSC Wilaya ya Chamwino Bi. Paulina Kanumba amewashukuru Walimu wakuu kwa ushirikiano wao na ofisi ya TSC kwa kueleza changamoto zao pamoja na kujenga mazingira bora ya kufanya kazi kwa amani.
Akihitimisha kwa kutoa neno la shukrani katika hafla hiyo kwa niaba ya Mkurugeni Mtendaji, Mganga Mkuu wa Wilaya ya Chamwino Dkt. Eusebi Kessy amehaidi ofisi ya Mkurugenzi kuendelea kutoa ushirikiano kwa ofisi ya TSC ili kuweza kufanikisha utekelezaji wa majukumu yao.
Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino
Sanduku la posta: 1126 Dodoma
Simu ya Mezani: 026 296 1511
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@chamwinodc.go.tz
Hakimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino. Haki zote Zimehifadhiwa.