Na Brian Machange- Chamwino
Ofisi ya TARURA Wilaya kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino imewezesha kutoa elimu ya kinga dhidi ya maambukizi ya ugonjwa wa UKIMWI kwenye mradi wake wa ujenzi wa barabara unaotekelezwa katika Kata tatu za Idifu, Nghahelezi na Manzase Wilayani Chamwino kwa kipindi cha robo ya tatu 2021.
Hayo yamesemwa na Makamu Mwenyekiti wa Halmashauri hiyo Mhe. Kenneth Yindi alipokuwa akitoa taarifa ya utekelezaji wa shughuli zilizotekelezwa na kamati ya kudhibiti ukimwi kwa kipindi cha robo ya Januari hadi Machi 2020/2021,kwenye kikao cha Baraza la madiwani kilichofanyika wilayani Chamwino.
Amesema kuwa Halmashauri hiyo kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imeendelea kutekeleza majukumu yake ya mapambano dhidi ya VVU na UKIMWI ili iweze kufikia malengo ya sifuri tatu ifikapo mwaka 2030,
Halmashauri ya wilaya ya Chamwino kwa kushirikiana na Tume ya kudhibiti ukimwi na shirika lisilo la kiserikali la TAYOA limesambaza jumla ya makasha 508 yenye kondom 10,200 kwenye kata 25 za wilaya hiyo kwa kipindi cha miezi mitatu mwaka 2021.
Mheshimiwa Yindi ambaye pia ni diwani wa kata ya Buigiri alitaja kata ambazo zilizosambaziwa makasha hayo ya kondom ni pamoja na Nhinhi, Mlowa Bwawani, Manzase, Chiboli, Fufu, Loje, Mpwayungu na Nghambaku.
Kata zingine ni Chinugulu, Huzi, Manda, Chilonwa, Membe, Dabalo, Itiso, Segala, Chamwino, Buigiri, Msanga, Manchali, Handali, Igandu, Nghahelezi, Mvumi Misheni na Mlowa Barabarani.
Makamu huyo alisema kuwa kwa upande wa huduma ya tiba kwa magonjwa ya ngono na kinga kwa ajili ya kuzuia na kusambaa hutolewa katika vituo vipatavyo 70 vilivyopo katika Halmashauri na kwa kipindi cha miezi mitatu jumla ya wateja 2050 walijitokeza huku wanawake wakiwa 1050 na wanaume 1000.
Hata hivyo alisema kuwa bado kuna changamoto kwa kamati za kudhibiti UKIMWI ndani ya kata kutowasilisha kikamilifu taarifa za utekelezaji za kila robo mwaka kutokana na kutotilia mkazo athari za maambukizi ya virusi.
Aidha kwenye kikao hicho, Madiwani viti maalumu wameiomba Halmashauri hiyo pamoja na taasisi zisizo za kiserikali kuhakikisha wanasambaza pia kondom za kike ili kulingika kundi hilo na maambukizi ya virusi vya UKIMWI kama ilivyo kwa wanaume.
Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino
Sanduku la posta: 1126 Dodoma
Simu ya Mezani: 026 296 1511
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@chamwinodc.go.tz
Hakimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino. Haki zote Zimehifadhiwa.