Kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Lishe Kitaifa kwa mwaka 2021 yanatarajiwa kuadhimishwa ifikapo Oktoba 23, Mkoani Tabora ambapo kwa mwaka huu yataambatana na shughuli mbalimbali ikiwemo maonesho ya Afya na lishe yatakayofanyika katika Viwanja vya Nane nane Ipuli mkoani humo.
Akizungumza katika Mkutano na Waaandishi wa habari Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania Dkt. Germana Leyna katika ukumbi wa Mikutano wa Taasisi hiyo amesema maadhimisho ya Mwaka huu yamebebwa na Kauli Mbiu isemayo “Lishe Bora ni Kinga Thabiti dhidi ya Magonjwa: Kula Mlo Kamili , Fanya Mazoezi, Kazi Iendelee”
Dr Germana amesema lengo la kuanzisha Siku ya Lishe ya kitaifa ni kuwaleta kwa pamoja wadau wa lishe ambao ni viongozi, wanasiasa, watendaji, wataalamu, wadau wa maendeleo, mashirika yasiyo ya Kiserikali na wananchi ili kuongeza ufahamu kuhusu umuhimu wa lishe kama msingi wa afya bora na maendeleo ya kiuchumi na kijamii.
“Ndugu zangu wanahabari Siku ya Lishe Kitaifa itatanguliwa na na shughuli mbalimbali ikiwemo kutoa elimu kwa jamii juu ya utayarishaji wa mlo kamili kwa makundi mbalimbali wakiwemo watoto, vijana, wajawazito, wanawake wanaonyesha, wazee, wagonjwa pamoja na watu wengine, kufanya uchunguzi wa afya na lishe kwa watu wote pamoja na kutoa ushauri stahiki bila kusahau kufanya maonesho ya bidhaa/ vyakula vilivyoongezewa virutubishi. alisema Dkt.Germana.
Maadhimisho ya Siku ya Lishe Kitaifa kwa mwaka huu ni ya pili tangu kuanzishwa kwake ambapo kwa mara ya kwanza yalifanyika Mwaka 2020 Mkoani Dodoma, ambapo siku hii imetajwa kutumika kama jukwaa muhimu katika kutekeleza na kuendeleza azma ya Serikali ya kutokomeza aina zote za utapiamlo nchini na kuongeza uelewa na ufahamu juu ya lishe bora na hatua madhubuti zinazopaswa kuchukuliwa na wananchi ili kuleta mabadiliko chanya hususani katika ngazi ya jamii.
Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino
Sanduku la posta: 1126 Dodoma
Simu ya Mezani: 026 296 1511
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@chamwinodc.go.tz
Hakimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino. Haki zote Zimehifadhiwa.