Shirikisho la watanzania waishio nchini Sweden (SHIWATASWE) limekabidhi Jumla ya miche ya miti ya matunda 400 katika shule ya Msingi chamwino Kwa Ajili ya kuunga mkono juhudi za Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Wa Jamhuri ya Muungano Wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan katika kampeni ya kukijanisha jiji la Dodoma ili kuhuisha shughuli za utunzaji Wa Mazingira.
Akizingumza wakati Wa zoezi Hilo lililofanyika Leo Disemba 5 , 2023 katika viwanja vya shule ya Msingi Chamwino iliyopo Halmashauri ya Chamwino Mkoa wa Dodoma Mwakilishi Wa shirikisho Hilo ambaye ni Katibu Bi.Martha Kente amesema kuwa miche hiyo imegawanyika katika makundi kadhaa ikiwemo miche ya Miembe 200, Mipera 40, Michungwa 80 , Mipapai 60 na Miparachichi Miche 30.
Alisema zoezi Hilo limekuja kufuatia Ofisi ya Makamu Wa Rais Wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Dkt.Philip Isidory Mpango kupitia Wizara ya Ofisi ya makamu wa Rais Muungano na Mazingira kusisitiza zoezi la upandaji miti hivyo Kwa umoja wao wanadiaspora hao wameamua kutia nguvu kwenye suala hilo.
Akisema moja ya lengo lao ni kuwaona wanafunzi wanajifunza kwa vitendo kutunza mazingira hivyo watakuwa na ushirikiano wa mwaka mmoja na shule hiyo kwa ajili ya kufuatilia zoezi hilo huku akiwaomba wanafunzi kuitunza vyema miti hiyo ili wafaidi matunda yake.
Ametoa shukrani zake za dhati Kwa serikali kupitia balozi wa Tanzania nchini Sweden, Wizara ya mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Kwa kuwasaidia kufanikisha adhma Yao, sambamba na kuupongeza uongozi Wa shule ya Msingi Chamwino Kwa kuridhia na kupokea Mpango huo huku akiwasisitiza kuitunza miti hiyo kwakuwa watafanya ufuatiliaji wa kina ili kuhakikisha adhma yao ya kukijanisha eneo Hilo inatimia.
"Kwanza kabisa nitie shukrani zangu Kwa serikali ya Jamhuri ya Muungano Wa Tanzania chini ya Rais wetu, mama yetu mpendwa Mh. Dkt. Samia Suluhu Hassan, pili Kwa Wizara ya mambo ya nje na ushirikiano wa Afrika mashariki Kwa kutusaidia kutuunganisha na uongozi Wa shule hii, lakini pia tunawashukuru viongozi wa shule ya Msingi Chamwino Kwa kuridhia ombi letu, niwaombe muitunze miti hii ambayo tumeileta kwa ajili ya kuunga mkono juhudi za Serikali katika utunzaji mazingira lakini niseme tu miti hii pia itakuwa na umuhimu mkubwa kwa wanafunzi kwani watapata matunda na kuimarisha afya zao" amesema Martha.
Kwa upande wake Afisa Elimu Taaluma wilaya ya chamwino ambaye pia alimwakilisha Mkurugenzi wa Halmashauri Mwl. Happyness Mugongo amewashukuru SHIWATASWE kwa uamuzi bora wa kushiriki zoezi la utunzaji Mazingira licha ya kuishi ughaibuni.
Pia ameeleza kuwa zoezi hilo limekuja wakati muafaka ambapo tangu mwaka jana Serikali kupitia kampeni ya kijanisha Dodoma ilipanda miti ya kutosha katika shule za misingi pekee ilipanda miti elfu tano(5,000) na mpaka sasa miti 4200 inaendelea vizuri. Mwl. Mugongo pia amesema wizara husika imetoa nafasi ya shule tano za mfano kupanda miti ambapo anatarajia kupokea miti 500 itakayopandwa katika shule hizo.
Katika hatua nyingine Bi.Mugongo ambaye pia ni mratibu wa zoezi la upandaji miti katika shule za msingi aliandika maombi kuomba ufadhili katika mfuko wa misitu unaofadhili shule nne (shule tatu za msingi na shule moja ya sekondari) na kufanikiwa kuanzisha vitalu vya uzalishaji wa miche hiyo kwa ajili ya kuisambaza katika maeneo mengine ikiwemo taasisi za shule, makanisa, n.k kwa lengo la kufanikisha kampeni ya kukijanisha Dodoma pamoja na juhudi zingine zinazoendelea.
Katika hatua nyingine amewaahidi kuwa atasimamia suala la utunzaji wa mimea hiyo ili kutimiza Adhma yao kwakuwa yeye pia ni mdau Wa Mazingira.Pia amewaomba kuangalia namna ya kuwasaidia wanafunzi Wa shule ya Msingi Chamwino kuondokana na changamoto ya ukosefu wa Maji inayowakabili kipindi cha kiangazi ili waweze kuitunza miti hiyo vyema kwakuwa changamoto hiyo inaweza kuwa kikwazo cha kufikia lengo la kuitunza na kulinda miti hiyo.
“najua nyie mpo na mna wadau wengi , changamoto yangu kubwa katika shule hii ya msingi Chamwino ambayo ipo katika uso wa Halamashauri ni maji, watoto wanapata taabu sana kipindi cha kiangazi kwakuwa Dodoma ni kame , kwahiyo nawaomba kama mnaweza kutusaidia kupata neema ya maji mkirudi mtakuta shule ya msingi Chamwino syo hii mnayoiona kwasababu naiamini timu yangu inayofanya kazi hapa walimu wangu hawatoniangusha, kama itatokea neema ya namna yeyote ya kupata maji kwakweli mtatusaidia sana katika kutunza miti wakati wa kiangazi kwakweli nawashukuru sana na ninaimani mtatusaidia”
Naye Mwalim mkuu Wa shule hiyo Mwl. James Kifaru ameonesha kufurahishwa na kitendo hicho maradufu, akiahidi kuwa Mstari wa mbele katika kuitunza na kulinda miche hiyo mpaka itakapokua Kwa kuimwagilia na kutilia mbolea.Ameongeza kuwa kitendo hicho kitasaidia kuwafundisha watoto juu ya umuhimu Wa utunzaji wa Mazingira na namna ya kulinda miti.
Tukio hilo la kizalendo limehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali ngazi ya Halmashauri, kata na kijiji cha Chamwino pamoja na viongozi wa shule hususani kamati ya shule, waalimu, wanafunzi na baadhi ya wazazi.
Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino
Sanduku la posta: 1126 Dodoma
Simu ya Mezani: 026 296 1511
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@chamwinodc.go.tz
Hakimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino. Haki zote Zimehifadhiwa.