Mkuu wa Wilaya ya Chamwino Mhe. Gift Isaya Msuya amefanya mkutano wa hadhara na wananchi wa kata ya Membe Novemba 13, 2023 kwa lengo la kutatua sintofahamu iliyoibuliwa na wananchi wa vijiji vya Membe na Chitabuli wakihofia Serikali kuchukua maeneo yao na kukosa mahali pa kulima.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti wananchi hao walitaka kufahamu iwapo mradi wa umwagiliaji utapoanza kutelezwa waliokuwa na maeneo kama wataendelea kulima kwenye maeneo yao au watanyang'anywa na kupewa watu wengine.
Vile vile walitaka kujua ekari 2500 watakazopewa wananchi kulima maana tayari wako kwenye maandalizi ya kuandaa mashamba kwa ajili ya msimu unaokuja.
Akijibu hoja zao Mkuu wa Wilaya alianza kwa kueleza kuhusu sheria na taratibu za umiliki wa ardhi kutoka ngazi ya kijiji hadi ngazi ya juu.
" utaratibu uliowekwa kisheria Serikali ya kijiji imepewa mamlaka ya kutoa kwa mtu mmoja mmoja ardhi isiyozidi ekeri 50. Na ikizidi ekari 50 hadi 1000 imepewa Baraza la madiwani kutoa kibali cha ardhi hiyo kutumika na mtu mmojammoja, ama shirika, ama kampuni ama taasis. Ikizidi ekari 1000 inakwenda kwa kamishina wa ardhi ambaye amekasimiwa na ya Tanzania kusimamia ardh.i" Alisema Mkuu wa Wilaya.
" Tunapokuja kwenye ardhi ya kijiji Serikali inapotaka kutekeleza mradi, Serikali ya kijiji inatakiwa ikae kikao, itaonyesha eneo la kutekeleza mradi na itaandika muhtasari wa kikao cha Halmashauri kuu ya kijiji lkn itapeleka muhtasari wa mkutanomkuu wa kijiji wananchi walioridhia eneo hilo lifanyike uwekezaji wa kitaifa." Alisema Mkuu wa Wilaya
Aidha aliendelea kueleza kuwa kwa membe jambo hilo limeanza tangu 2018 na 2021 nyaraka za mkutano zilionyesha eneo hilo limekubaliwa kuwa ni shamba na Halmashauri ilikaa vikao vyake na kupitisha ekari 8000 kwa ajili ya uwekezaji wa kilimo na kuanzia hapo tunapeleka kwa kamishina na kusajili hiyo ardhi na kwa mujibu wa sheria inakuwa ni ardhi inayosimamiwa na Halmashauri kwa ajili ya uwekezaji wa kilimo.
Vilevile alieleza kuwa Chamwino imepata upendeleo kwa kupelekewa miradi hii na Mhe. Rais Mama Samia Suluhu Hassan kwani ingeweza kupelekwa sehemu nyingine.
"Sisi Chamwino na Dodoma tumependelewa sana na nisingetegemea miradi hii ilete huzuni bali nilitegemea miradi hii ilete furaha kwa wananchi." Alisema Mkuu wa Wilaya.
Kuhusu wananchi kuondolewa kwenye maeno Mkuu wa wilaya alieleza kuwa hakuna mwananchi yeyote atakayekuwa na eneo kwenye eneo la mradi atanyang'anywa shamba bali wote watapewa maeneo baada ya Serikali kujiridhisha na nyaraka za umiliki wa maeneo kwenye eneo hilo la mradi.
Aliendelea kueleza kuwa Serikali inayodhamira njema kwa wananchi na lengo la mradi ni kwa ajili ya kuwainua wanachi kiuchumi na hivyo mbali na ekari zitakazokuwa chini ya Serikali ambazo zitagawiwa kwa vijana ambao tayari wapo kwenye mafunzo kwa ajili ya kujifunza kilimo cha kisasa, wananchi wametengewa ekari 2500 ambazo watagawiwa kulingana na ukubwa wa maeneo wanayomiliki.
"Waziri bashe ameelekeza wale wote waliokuwa na mashamba kwenye eneo hilo wapewe maeneo ndani ya shamba kulingana na ukubwa wa maeneo yao. Watakachofanya watahakiki kaya zote, kila kaya itapewa eneo la kulima ndani ya mradi." Alisema Mkuu wa Wilaya.
Mkuu wa wilaya alieleza faida zitakazopatikana kupitia mradi huo ikiwemo kukinga maji yanayoshuka kwenye milima kipindi cha mvua ambayo husababisha mafuriko na uharibifu wa miundombinu na mali nyingine na kujenga uchumi wa wakazi wa Wilaya ya Chamwino.
Mwisho kupitia Mkutano huo yaliwekwa maazimio ambayo yatapaswa kukamilishwa ndani ya wiki moja na wiki ijayo watakutana tena kwa ajili ya kupitia utekelezaji wa maazimio hayo.
Mkutano huo ulihudhuriwa na Mwenyekiti wa Wilaya wa Chama cha Mapinduzi Mhe. Malima mwakilishi wa Mkuu wa mkoa wa Dodoma Bibi Aziza Mumbana wataalam toka Tume ya Umwagiliaji wanosimamia mradi.
Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino
Sanduku la posta: 1126 Dodoma
Simu ya Mezani: 026 296 1511
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@chamwinodc.go.tz
Hakimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino. Haki zote Zimehifadhiwa.