Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Staki Senyamule amefanya ziara ya kukagua miradi ya maendeleo na kusikiliza kero za wananchi Wilayani Chamwino Septemba 14, 2023.
Ziara imefanyika kwenye kata za Manchali ambapo amekagua ujenzi wa shule mpya ya wasichanaya mkoa wa Dodoma na shule mpya ya Sekondari ya Kata ya Manchali, Mlowa Bwawani amekagua ujenzi wa chuo cha Veta na katika miradi hiyo yote alitoa maelekezo mbalimbali ya kufuata ili miradi yote iweze kukamilika kwa wakati na kwa ubora.
Vilevile aliwataka wananchi kuwa walinzi wa vifaavilivyopo eneo la mradi kwani kufanya hivyo kunaweza kupelekea miradi kushindwa kukamilika kwa ubora unaotakiwa.
"Kuweni walinzi, hakikisheni hakuna anayeiba kifaa hata kimoja katika eneo hili. Watoto wenu wengine ni vibarua hapa, hakikisheni harudi na kitu nyumbani ambacho amekitoa hapa.Msione furaha leo kwa mfuko mmoja anaopata lakini adha anayosababisha hapa ni kubwa ya kukosa uzalendo na mwisho wa siku kila Mtanzania ni mlinzi wa mali ya Umma na mwisho wapeni mafundi ushirikiano wote unaohitajika ili kazi kwao ziwe rahisi."
Baada ya kukagua miradi alifanya mkutano wa hadhara na wananchi kwenye kata ya Mlowa Barabarani kwa ajili ya kusikiliza na kutatua kero za wananchi. kero mbalimbali ziliwasilishwa ikiwemo suala la kuunda jumuiya ya watumia maji ambao watasimamia uendeshaji wa mradi wa maji ambalo wananchi walikuwa wakilipinga.
Aidha Mkuu wa mkoa amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano Mhe. Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuleta fedha kwa ajili ya miradi hiyo mikubwa nakueleza kuwa jambo hilo si la kubeza hata kidogo kwani maeneo yenye uhitaji ni mengi kwa mkoa mzima na kwa wilaya pia, lakini wao wamebahatika kupata fedha hizo.
"Endeleeni kuwaambia wengine mambo mazuri na kazi nzuri anazozifanya Mhe. Rais wetu mpendwa. amejitoa kwa ajili ya watanzania. Tumepata bahati shule mbili zinzjengwa kwenye Kata moja, hivyo mlione ni jambo la thamani na halijatokea kwa bahati mbaya. limetokea kwa sababu yupo mtu mmoja pale juu anaitwa Mhe Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambaye ameamua kufanya maendeleo kwa Watanzania. Mkisikia mtu anabeza vitu vya maendeleo muogopeni. Hatuna zawadi ya kumpa nyie mwambieni asante na ungeni mkono juhudi zake."
Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino
Sanduku la posta: 1126 Dodoma
Simu ya Mezani: 026 296 1511
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@chamwinodc.go.tz
Hakimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino. Haki zote Zimehifadhiwa.