Na Brian Machange - Chamwino
Naibu Waziri wa Kilimo, Mheshimiwa Hussein Bashe, ameagiza maboresho yafanyike kwenye Mradi wa Umwagiliaji Zabibu wa Chinangali uliopo wilayani Chamwino mkoani Dodoma unaosimamiwa na Chama cha Ushirika cha Chabuma AMCOS.
Mheshimiwa Bashe ameyasema hayo hivi karibuni alipotembelea Mradi huo wa umwagiliaji wa Zabibu uliokuwa haufanyi kazi kwa kipindi kirefu ambapo ametoa maelekezo kwa vyombo vyote vinavyohusika na mradi huu kuhakikisha unaanza kufanya kazi tena. Amemuagiza Mrajis wa Vyama vya Ushirka kufanya Semina katika chama hiki cha Chabuma AMCOS ili kutoa elimu juu ya ushirika na kutoa elimu ya Stakabadhi Ghalani kwa wanaushirika na wakulima kwa ujumla.
Naibu Waziri amewaagiza Mkurugenzi wa Wilaya ya Chamwino, Ndugu Athuman Masasi na Mrajis wa Vyama vya Ushirika na Mtendaji Mkuu wa Tume ya Maendeleo ya Ushirika, Dkt. Benson Ndiege, kuwaandikia barua wanachama wote wenye mashamba yao kwenye mradi huo kuyasafisha ndani ya siku thelathini (mwezi mmoja), na atayekiuka na kutosafisha shamba lake ndani ya siku hizo basi anyang’anywe shamba lake.
“Tume ya Umwagiliaji kesho walete wataalam watakaobadilisha mfumo wa mitambo kutoka kutumia umeme kwenda kutumia nguvu ya jua (solar system); na naitaka Tume ya Umwagiliaji kuweka kambi hapa shambani kwa gharama zake ili iweze kufanya uchunguzi wa vifaa vinavyotumika kwenye umwagiliaji katika mashamba haya,” amesema Mhe. Bashe.
Naibu Waziri wa Kilimo ameitaka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo (TARI), ndani ya miezi minne kuleta miche ya Zabibu kwa wanachama wenye mashamba yao kwenye mradi huo na amewataka wakulima katika kipindi cha kusubiri miche waweze kufanya kilimo cha Karanga kwenye mashamba hayo.
Aidha, Mhe. Bashe amemtaka Mkuu wa Wilaya ya Chamwino, Bi. Vumilia Nyamoga, kusimamia kurejeshwa kwa transfoma lililoondolewa kwenye mradi huo na ameagiza TAKUKURU kusimamia kurejeshwa kwa Shilingi milioni 150 zilizokopwa na Chabuma AMCOS kutoka ALKO Vintage.
“Hii ni mara ya mwisho kuwainua tena, Serikali haitaingilia mradi wowote mtakaouharibu kwa makusudi; tumeshaweka mkakati mzuri wa kibiashara na tumetafuta mnunuzi yuko hapa, Alko vintage ambaye ameahidi kununua Zabibu zote zitakazolimwa. Vilevile, Benki ya CRDB tutakaa nao meza moja tuone namna ya kuweza kulipa deni la Shilingi bilioni 2.4 wanazodai kwa Chabuma AMCOS, nawahakikishia wakulima hakuna atakayeumia na deni hili,” alisema Naibu Waziri wa Kilimo.
Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino
Sanduku la posta: 1126 Dodoma
Simu ya Mezani: 026 296 1511
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@chamwinodc.go.tz
Hakimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino. Haki zote Zimehifadhiwa.