Naibu Waziri Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Khamis Hamza Khamis amefanya ziara ya kukagua shughuli za uchimbaji wa madini katika eneo la msitu wa hifadhi wa Chinyami kijiji cha Nayu kata ya Dabalo Wilayani Chamwino.
Ziara hiyo imefanyika leo Agosti 10,2022 ambapo alikutana na kufanya mazungumzo na wawekezaji ( wachimbaji wadogo) pamoja na wananchi wa eneo hilo.
Katika ziara hiyo Naibu waziri amebaini baadhi ya taratibu za uchimbaji kukiukwa na hivyo ametoa maelekezo kwa wachimbaji hao wayatekeleze ndani ya mwezi mmoja na ikiwa watashindwa kufanya hivyo watafungiwa kuendelea na shughuli hizo za uchimbaji.
Mhe. Naibu waziri ameelekeza wachimbaji hao waende Taasis zote zinazohusika na utoaji wa vibali vya uchimbaji madini ikiwemo Wakara wa misitu(TFS), Bonde la maji Wami - Ruvu na NEMC waombe vibali.
"Nendeni kwenye taasis zote zinazohusika mkapate vibali. Tunataka uwekezaji wenye tija utakaokuwa na faida kwa wote." Amesema Naibu Waziri.
Vilevile Naibu Waziri ametoa mwezi mmoja kwa wachimbaji kutengeneza utaratibu mzuri wa kudhibiti maji yanayotumika kuosha dhahabu yasilete athari kwa binadamu na mazingira.
" Maji yenye sumu yanaweza kuleta magonjwa kama mapafu na miti inaweza isiote. Athari ya sumu huipati leo.Maji hayo yanatiririka na kwenda kwenye vyanzo vya maji na watu wanayatumia kulima, kufuga samaki, kunywa, kuoga." Amesema Naibu Waziri.
Rai pia imetolewa kwa wote wanaotorosha madini na ameomba waache mara moja na badala yake madini yanayopatikana kwenye eneo hilo yauzwe kwenye masoko ya madini ili kuiwezesha Serikali kupata mapato.wanaotorosha madini watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria.
"Serikali yetu inahitaji mapato. Kuna watu wanatorosha madini. Kuna masoko ya kuuzia madini. Jambo hilo liachwe, kauze madini sehemu halali inayohusika. Ukitorosha sheria itakuandama." Amesema Naibu Waziri.
Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino
Sanduku la posta: 1126 Dodoma
Simu ya Mezani: 026 296 1511
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@chamwinodc.go.tz
Hakimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino. Haki zote Zimehifadhiwa.