Mkuu wa Wilaya ya Chamwino Mheshimiwa Vumilia Nyamoga amekabidhi hati miliki za kimila kwa wakulima wa maembe wa kijiji cha chifukulo hivi karibuni kwenye hafla iliyofanyika kijijini hapo.
Ilielezwa mradi huu wa kuandaa mpango wa matumizi ya ardhi katika kijiji cha Chifukulo unafadhiliwa na kampuni ya Local Investiment Climate na mpaka sasa jumla ya hati miliki za kimila 175 zimeandaliwa na zimekamilika.
Katika hotuba yake Mkuu wa Wilaya amewataka wakulima kutokubeza uwekezaji huo wa shamba la maembe na badala yake ni vema kila kaya au familia ikawa na eneo kwenye shamba hilo, alisema ‘Isiwe ninyi mmetoa maeneo yenu ekari 500 kisha wao wakawa pembeni na wakafaidika wa pembeni kitu ambacho kitakuwa hakipendezi.’
Amewataka wayasimamie maeneo watakayopewa kwa uaminifu kwa kufuata kanuni za kilimo bora ili waweze kupata mazao mengi na watakapouza waweze kupata fedha za kujikimu na familia zao na kwa kufanya hivyo wana Chifukulo wana uhakika wa kuwa matajiri wa baadae. Amewaahidi wakulima kuwa kiwanda kitakapokuwa tayari na kwa kuwa ushirika tayari upo utawekwa utaratibu mzuri na bei ambayo itawanufaisha wakulima itawekwa
Alieleza kuwa kiwanda kwa ajili ya kusindika ‘juice’ kitakapojengwa maembe yaliyolimwa sasa hayataweza kukidhi mahitaji ya kiwanda hivyo alisisitiza wasiuachilie uwekezaji huo.
Akisoma taarifa kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji Wilaya Afisa Ardhi Mteule ndugu Letare Shoo alisema mradi huu wa kuandaa mpango wa matumizi bora ya ardhi , upimaji wa mashamba ya maembe umetumia Tshs. 52,538,900/=
Aidha alieleza kuwa maandalizi ya hati miliki nyingine yanaendelea ambapo wamiliki wa mashamba wanatakiwa kujaza fomu za utambuzi na kupigwa picha, zoezi ambalo linaendelea katika ofisi za LIC.
Vilevile alieleza kuwa kampuni ya ya LIC inafadhili uendelezaji wa shamba kwa kununua miche bora ya maembe ili ipandwe kwenye mashamba ya wanachama kwa lengo la kuboresha uzalishaji na ununuzi huo wa miche umegharimu kiasi cha Tshs. 37,500,000/=
Aidha ilielezwa kuwa katika kufanikisha ujenzi wa kiwanda katika eneo hili tayari hatua za awali zimeanza kutekelezwa kwa kuandaa andiko la mradi (business plan) kuainisha aina za mitambo itakayotumika, bidhaa zitakazozalishwa na michoro ya usanifu wa kiwanda.
Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino
Sanduku la posta: 1126 Dodoma
Simu ya Mezani: 026 296 1511
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@chamwinodc.go.tz
Hakimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino. Haki zote Zimehifadhiwa.