Mkuu wa mkoa wa Dodoma Mhe. Rosemary Sitaki Senyamule amefanya ziara ya kikazi wilayani Chamwino, Novemba 10, 2022 kwa lengo la kuzungumza na viongozi mbalimbali ngazi ya wilaya pamoja na watumishi na kukagua miradi ya maendeleo.
Akiwa kwenye kikao na viongozi hao pamoja na watumishi kilichofanyika kwenye jkumhi wa mikutano wa Halmashauri Mkuu wa Mkoa alipokea kero mbalimbali na zote zilipatiwa majibu.
Hoja zilizowasilishwa na kupatiwa majibu ni pamoja na soko la zabibu kusuasua na kuwa na bei ya chini na baadhi ya wakulima kutolipwa fedha zao mpaka sasa, ambapo majibu yalitolewa kuwa Serikali imeshaanza kulitafutia ufumbuzi suala la soko la zabibu.
Ilielezwa kuwa kwa mwaka huu wa fedha Serikali imetenga fedha kwa ajili ya kujenga kiwanda kwa ajili ya kukamua mchuzi wa zabibu ikiwa ni pamoja na kujenga matenki ya kuhifadhia mchuzi wa zabibu suala ambalo litapunguza adha hiyo.
Kuhusu suala la wakulima kutolipwa fedha zao ilielezwa kuwa tayari kampuni ya jambo wanaendelea kulipa na walichelewa kulipa kutokana na suala hilo la kununua kutokuwa kwenye mpango wao wa bajeti isipokuwa walifanya hivyo baada ya kuombwa na Serikali kununua zabibu ili kunusuru zisiharibikie shambani.
Kero nyingine ilikuwa ni kuhusu bwawa la Manchali ambalo limechimbwa tangu mwaka 1997 na tangu kipindi hicho halijawahi kufanyiwa ukarabati na tayari limejaa mchanga na kufanya shughuli za umwagiliaji kushindwa kufanyika.
Akijibu hoja hiyo Mkuu wa Idara ya Kilimo ndugu Godfrey Mnyamale alieleza kuwa bwawa hili limeshaandikiwa maandiko na WFP walielekeza uongozi wa kata kutunza mazingira ya bwawa na kutoruhusu mifugo kuingia na kuchunga kwenye eneo la bwawa na iwapo hayo yatatekelezwa kwenye bajeti ya 2023/2024 wataleta fedha kwa ajili ya kurikarabati.
"Wameshaandika maandiko, WFP walielekeza uongozi wa kata kusimamia kutunza mazingira ya bwawa na kutoingiza mifugo na bajetimya 2023/2024 wataleta fedha.' Alisema Mnyamale.
Kuhusu kero ya daraja la Chilonwa ambalo limesababisha ajali nyingi kipindi cha masika, afisa kutoka TANROAD alieleza kuwa kwenye bajeti ya mwaka huu wa fedha wa 2022/2023 Serikali imetenga fedha kwa ajili ya usanifu na kazi hiyo ya usanifu ambayo inatarajiwa kukamilika ifikapo mwezi Februari 2023, watatangaza tenda ya ujenzi wa daraja.
Naye Katibu Tawala wa Mkoa wa Dodoma Bibi Fatuma Mganga ameipongeza Halmashauri kwa kupata mradi wa bwawa kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji na ameielekeza Halmashauri kuweka mipango mizuri ili kuongeza mapato.
"Nawapongeza kwa kupata fursa za mabwawa kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji. Natarajia katika mradi wa bwawa mlioupata mipango iwe mizuri ili kuongeza mapato."Alisema Katibu Tawala Mkoa.
Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino
Sanduku la posta: 1126 Dodoma
Simu ya Mezani: 026 296 1511
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@chamwinodc.go.tz
Hakimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino. Haki zote Zimehifadhiwa.