Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Mheshimiwa Binilith Mahenge amefanya ziara ya siku mbili Wilayani Chamwino kwa lengo la kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo pamoja na kuongea na wananchi.
Ziara hiyo ilifanyika Julai 09, 2019 na kumalizika Julai 10, 2019 katika kata za Buigiri, Haneti na Manda.
Akiwa kata ya Buigiri alitembelea mradi wa shamba la zabibu na kuongea na wakulima wenye maeneo katika shamba hilo ambapo ilibainika kuwa mradi huo haufanyi vizuri kama ilivyotarajiwa.
Mkurugenzi Mtendaji Ndugu Athumani H. Masasi alieleza kuwa Halmashauri ililiona hilo na imejipanga kuuchukua mradi huo na kuuendesha wao wenyewe kama mradi wa kimkakati na ndani ya muda mfupi wataweza kupata faida na kuondokana na shida ya mapato.
Kutokana na maelezo hayo Mkuu wa Mkoa alimwagiza Mkurugenzi Mtendaji Wilaya kuteuwa kamati ndogo miongoni mwa wataalam wake ili washirikiane na wataalam wa Mkoa wakae na kuangalia namna bora ya kuendesha mradi huo ili uwe na tija kwa Halmashauri na wananchi. Ametaka mapendekezo hayo yawasilishwe kwake siku ya Jumatatu Julai 15, 2019.
Aidha Mkuu wa Mkoa ameelekeza kuwa wakulima hai waliopo kwenye mradi huo watambuliwe na iangaliwe namna ya wao kuendelea kuwepo kwenye mradi kwani wao ni wabia ambao wako tayari.
Akiwa Haneti Mkuu wa Mkoa amekabidhiwa mifuko 20 ya cementi na vikundi vya wachimbaji wadogo kwa ajili ya ujenzi wa madarasa katika shule ya Msingi kwa Hemu. Mkuu wa Mkoa amewashukuru wachimbaji wadogo hao kwa mchango walioutoa.
Akiwa kijiji cha Ilangali Kata ya Manda Mkuu wa Mkoa ameagiza jingo jipya la zahanati ya kijiji hicho iliyojengwa kwa ushirikiano na wananchi, Halmashauri na TANAPA ambayo imekamilika na inavifaa vyote ianze kutumika kuanzia Julai 11, 2019 na yeye atakwenda kuongea na Waziri wa Maliasili ili akafungue jengo likiwa linatumika.
“Haiwezekani jengo limekamilika lakini halitumiki, hivyo naelekeza kuanzia kesho julai 11,2019 jengo lianze kutumika na litafunguliwa likiwa linatumika”. Alisema Mkuu wa Mkoa.
Kuhusu changamoto ya ubovu barabara na uchache wa vyombo vya usafiri kwa wakazi wa Mandan na Ilangali Mkuu wa Mkoa amewaelekeza TARURA kuipa kipaumbele cha kwanza barabara hiyo miongoni mwa barabara zitakazotengenezwa katika bajeti ya mwaka wa fedha 2019/2020.
Vilevile alieleza kuwa Mkoa utaipa pia kipaumbele ili ijengwe kwa kiwango kizuri kwa kuwa ikitengenezwa vizuri itafungua fursa ya utalii kwa watalii watakaotembelea hifadhi ya Ruaha kwani itakuwa fupi na hivyo kuchagiza maendeleo kwa wannanchi wa maeneo hayo.
Kuhusu changamoto ya vyombo vya usafiri ametoa maelekezo kwa Mkurugenzi Mtendaji Wilaya na Mkuu wa Wilaya kuwasiliana na SUMATRA kuomba idhini ya kutangaza ili kupata wamiliki wengine wa vyombo vya usafiri watakaopeleka mabasi.
“Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi shirikianeni mfanye mawasiliano na SUMATRA mtoe tangazo ili wadau wengine ili wadau wengine waweze kuleta mabasi.” Alisema Mkuu wa Mkoa.
Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino
Sanduku la posta: 1126 Dodoma
Simu ya Mezani: 026 296 1511
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@chamwinodc.go.tz
Hakimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino. Haki zote Zimehifadhiwa.