Taasisi isiyo ya Kiserikali ya Aga Khan nchini Tanzania imetambulisha mradi wa “Tuinuke Pamoja” mbele ya timu ya Menejimenti ya Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino leo tarehe 2 Julai, 2025 katika ukumbi mdogo wa ofisi ya Mkurugenzi.
Mradi huo unatekelezwa na taasisi ya Aga Khan kwa kushirikiana na mtandao wa jinsia nchini Tanzania TGNP (Tanzania Gender Networking Program) chini ya ufadhili wa Ubalozi wa Ireland nchini Tanzania.
Akiutambulisha mradi huo mwakilishi kutoka taasisi ya Aga Khan Ndugu Nestory Florian Mhando, amesema lengo la mradi huo ni kuhuisha nguvu za pamoja za vikundi vya kijamii ili kuweza kufikia usawa wa kijinsia na kumwezesha mwanamke.
Halikadhalika, mradi wa Tuinuke Pamoja umelenga kufikia vikundi mbalimbali vya kijamii ndani ya Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino katika sekta ya afya, elimu, mazingira pamoja na kilimo.
Kwa upande wake Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino Dkt. Eusebi Kessy ameiasa taasisi ya Aga Khan kupitia mradi wa Tuinuke Pamoja kuhakikisha wanaandaa njia bora ya kubainisha vikundi vitakavyonufaika na mradi huo ili makundi muhimu yakiwemo ya afya hayaachwi nyuma katika mradi huo.
Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino
Sanduku la posta: 1126 Dodoma
Simu ya Mezani: 026 296 1511
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@chamwinodc.go.tz
Hakimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino. Haki zote Zimehifadhiwa.