Mkuu wa Mkoa ametoa maelekezo mbalimbali kwa watendaji wa Serikali ikiwemo suala la Elimu ambapo alisema bado ufaulu wa mkoa upo chini, upungufu wa miundo mbinu, utoro, mimba mashuleni na wanafunzi kuolewa wakiwa bado mashuleni.
Maelekezo hayo ameyatoa alipofanya ziara ya kikazi Wilayani Chamwino Novemba 10, 2022 iliyokuwa na lengo la kuzungumza na viongozi hao na watumishi pamoja na kukagua miradi ya maendeleo.
Aliwataka wadau wote wa elimu wafanye vikao kuanzia ngazi ya kata hadj wilaya na kufanya tathimini kuhusu elimu kwenye maeneo yao. Aliwataka viongozi kuongea na wananchi kuhusu kuunga mkono ujenzi wa miundombinu ya shule kwani Serikali imeshafanya sehemu kubwa.
Kuhusu kilimo mkuu wa mkoa ameelekeza kipewe kipaumbele na kukiwekea mikakati mizuri kwani 72% ya wananchi ni wa kulima. Alisema Mhe. Rais Mama Samia Suluhu Hassan amefanya kazi kubwa kwenye kilimo, alitolea mfano pikipiki zilizotolewa kwa maafisa ugani nchi nzima pamoja na miradi mingine ikiwemo ya umwagiliaji na hivyo wanamshukuru sana. Alisisitiza maafisa ugani wasimamiwe.
Vilevile Mkuu wa Mkoa alisisitiza kuhusu suala la uwajibikaji kwa watumishi wa umma ili kuleta matokeo yenye tija kwani Serikali imewekeza fedha nyingi kwenye mishahara ya watumishi.
"Watumishi Serikali inatuthamini sana na ndio maana inatulipa mishahara. Fedha nyingi imewekwa kwenye mishahara, hivyo ni lazima tuwajibike kwani Serikali inatutegemea tulete tija."
Kuhusu utawala bora alielekeza vikao vyote vya kisheria vya kijij na kata viwe vinafanyika na agenda ziwe zinazotakiwa. Kusimamia maadili ya watumishi. Taarifa za miradi zitolewe kwa wananchi. Kusikiliza kero za wananchi ikiwa ni pamoja na kuweka mazingira mazuri ya kupokea kero hizo.
Mkuu wa mkoa pia alitembelea mradi wa shamba la zabibu Chinangali wenye hekari 6000 ambao unatarajiwa kuanza upandaji hivi karibuni.
Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino
Sanduku la posta: 1126 Dodoma
Simu ya Mezani: 026 296 1511
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@chamwinodc.go.tz
Hakimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino. Haki zote Zimehifadhiwa.