Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino Ndugu A. H. Masasi ameitaka jamii ya Chamwino kuzingatia lishe bora kwa watoto na kuwaepusha na udumavu ili kujenga taifa lenye watu wenye afya bora.
Kauli hiyo ameitoa leo Ijumaa tarehe 06 Septemba, 2019 kwenye ukumbi wa Buzwagi uliopo Chamwino Ikulu wakati akifunga warsha ya kuwasainisha mikataba Watendaji wa Kata za Wilaya ya Chamwino inayowataka kwenda kusimamia utoaji wa elimu ya lishe kwenye vijiji kupitia wataalam wa afya.
Pamoja na kusaini mikataba hiyo wataalam wa lishe kutoka ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino wametoa maelekezo mbalimbali kwa Watendaji wa Kata ili kuwajengea uwezo wa kutekeleza jukumu hilo kwa ufanisi mkubwa.
Kwa upande wake Bw. Philimon Nsodya meneja wa Mradi wa Boresha Lishe (TAHEA) unaotekeleza shughuli za Shirika la Save the Children International amewataka Watendaji wa Kata kuzingatia maelekezo yote yaliyotolewa na amesema TAHEA iko tayari wakati wowote kushirikiana na Halmashauri ya Chamwino kuhakikisha elimu ya lishe inawafikia wananchi kwenye ngazi ya jamii.
Akizungumza baada ya kusaini mikataba, Mtendaji wa Kata ya Buigiri Bw. Matimba Pascal John amesema kuwa yeye na watendaji wenzake wa Kata wamepata uelewa wa kutosha na wako tayari kwenda kusimamia utekelezaji katika maeneo yao.
Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino
Sanduku la posta: 1126 Dodoma
Simu ya Mezani: 026 296 1511
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@chamwinodc.go.tz
Hakimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino. Haki zote Zimehifadhiwa.