Mkuu wa Wilaya ya Chamwino Mh. Janeth Mayanja ameagiza watendaji wa kata kuhakikisha wanafanya siku za lishe vijijini.
Mh. Mayanja ametoa maagizo hayo wakati akiongoza kikao cha robo ya kwanza cha lishe katika Wilaya ya Chamwino kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri.
Siku hizo za lishe ambazo hutakiwa kufanyika kila baada ya miezi mitatu katika vijiji zimetajwa kuwa ni muhimu kwa ajili ya kuleta uelewa kwa wananchi ili waweze kuzingatia hatua za lishe. Aidha, DC Mayanja amewataka watendaji hao kuhakikisha taarifa za lishe zinabandikwa katika mbao za matangazo ya vijiji na wanashiriki katika siku ya lishe katika kila kijiji ndani ya kata zao.
Akizungumzia katika suala la chakula shuleni, Mh. Janeth Mayanja amewataka watendaji ngazi ya kata na vijiji kuhakikisha wanakaa na wazazi na kutafuta namna nzuri ya kuchangia chakula shuleni ili kuhakikisha wanafunzi wote katika shule za Wilaya ya Chamwino wanapata chakula muda wa shule na sio tu kwa madarasa ya mitihani pekee.
Sanjari na hilo, ameshauri kutolewa kwa zawadi kwa shule na kata zote ambazo wanafunzi wake wote wanapata chakula shuleni. Aidha, ameahidi kuanzia kikao kinachofuata kupitia ofisi ya Mkuu wa Wilaya ataanza kutoa motisha kwa shule ambazo wanafunzi wake wanapata chakula shuleni.
Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino
Sanduku la posta: 1126 Dodoma
Simu ya Mezani: 026 296 1511
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@chamwinodc.go.tz
Hakimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino. Haki zote Zimehifadhiwa.