MHE.DKT PHILIP MPANGO AHIMIZA WANANCHI KUCHANGAMKIA FURSA ZA MAZAO MAPYA.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Dkt Philip Isdor Mpango amesisitiza wananchi kuchangamkia fursa za mazao mapya yanayostawi vizuri katika ardhi ya Dodoma na kuachana na dhana ya mkoa wa Dodoma ni nusu jangwa kwani mkoa huo umebarikiwa kuwa na kiasi kikubwa cha maji.
Akizungumza wakati akihitimisha ziara ya siku nne mkoani Dodoma katika mkutano wa hadhara Mpwayungu wilayani Chamwino Agosti 22, 2024, amesema mazao hayo mapya ya mitende, mizeituni, komamanga, karanga za miti na parachichi kuwa ni fursa adhimu kwa wananchi kujikwamua kiuchumi na kupunguza uagizaji wa baadhi ya mazao hayo kutoka nje ya nchi ikiwemo zao la tende. Hata hivyo, amesisitiza pia fursa katika kilimo cha kimkakati cha zabibu, alizeti, mbogamboga na mpunga.
Aidha, Mh. Dkt Philip Mpango ameweka jiwe la msingi katika mradi wa kilimo wa jenga kesho iliyobora (BBT) na kuwapongeza wananchi na viongozi wa vijiji vya Mlazo na Ndogowe wilayani Chamwino kwa kutoa ardhi ya ujenzi wa mradi huo mkubwa wa skimu ya umwagiliaji iliyopewa jina la Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Pia wizara ya kilimo imesisitizwa kuhakikisha jamii ya wafugaji nayo inanufaika na mradi huo mkubwa wa umwagiliaji pamoja na kuitaka wizara ya mifugo kuanzisha mradi wa jenga kesho iliyobora (BBT) kwa wafugaji kwa kutengewa eneo na kuwekewa miundombinu ya malisho.
Kwa upande wa Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mh. Mary Prisca Mahundi (mb) ameeleza wizara hiyo kuwa mbioni kutekeleza ujenzi wa miradi mikubwa ya kuboresha mawasiliano nchi nzima na kwa mkoa wa Dodoma minara mingi ya mawasiliano kujengwa ikiwemo wilaya ya Chamwino ambayo itanufaika na ujenzi wa minara 50.
Mh Naibu Waziri pia amempongeza mkuu wa wilaya ya Chamwino Mh. Janeth Mayanja kwa kushirikiana vyema na wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari kwaajili ya ujenzi wa minara katika maeneo ya Chiboli, Mlowa Bwawani na Ilangali wilayani Chamwino.
Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino
Sanduku la posta: 1126 Dodoma
Simu ya Mezani: 026 296 1511
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@chamwinodc.go.tz
Hakimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino. Haki zote Zimehifadhiwa.