Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino Ndg: Tito P. Mganwa leo Oktoba 07, 2024 amefunga mafunzo kwa Maafisa maendeleo na Maafisa watendaji wa Kata ambao ni wasimamizi wa mikopo ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu (10%) ngazi ya kata. Mikopo hii inatarajiwa kuanza kutolewa hivi karibuni kwa Vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, ambayo ilisitishwa na sasa kuja na utaratibu mpya ulioboreshwa wa utoaji wa mikopo hiyo.
Akizungumza alipokuwa akifunga mafunzo hayo amewaelekeza wasimamizi hao kwenda kuwaelimisha vizuri wananchi ikiwa ni pamoja na kuwaeleza ukweli kuhusu mikopo hiyo ili wanapofikia uamuzi wa kuchukuwa mkopo wachukuwe wakiwa na uelewa mzuri na hiyo itasaidia kuwa na urejeshaji mzuri wa mikopo watakayochukua.
"Suala la mikopo ni suala gumu kwa kuanzia kwa sisi wenyewe. Tunapokopa tunakuwa na changamoto. Mtu anapokopa anakuwa na wazo la biashara lakini anapoingia kwenye biashara yenyewe wakati mwingine inakuwa changamoto. Kwa hiyo inahitaji ushauri wa hali ya juu.Mara nyingi tumekuwa tunatoa mafunzo ambayo ni ya ujumla lakini waambieni watu ukweli toka mwanzo kuwa watapaswa kurejesha lakini pia tusaidie kwenye usimamizi kwa kufanya ufuatiliaji wa mara kwa mara." Alisema Mganwa.
Vilevile aliwaonya wasimamizi hao kutoruhusu siasa kwenye utoaji wa mikopo
"Kikubwa msiruhusu kamwe siasa iingie kwenye utoaji wa mikopo hii. Fuateni utaratibu, nyie siyo wanasiasa.Serikali imeweka utaratibu mzuri kabisa wa utoaji wa mikopo hii." Alisema Mganwa.
Aidha Mkurugenzi Mtendaji alielekeza wataalam wote ngazi ya kata washirikiane kusimamia miradi ya maendeleo iliyopo kwenye maeneo yao, wasiwaachie watendaji peke yao.
Mwisho kabisa wasimamizi hao walipewa kiapo kuhusu utoaji wa mikopo hii ya Serikali kilichotolewa na Mwanasheria wa Halmashauri Bibi Olipa Mkuyu.
"Serikali za Mitaa Sauti ya Wananchi, Jitokeze Kushiriki Uchaguzi"
Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino
Sanduku la posta: 1126 Dodoma
Simu ya Mezani: 026 296 1511
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@chamwinodc.go.tz
Hakimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino. Haki zote Zimehifadhiwa.