Mkuu wa Wilaya ya Chamwino Mhe. Janeth Mayanja ameongoza kikao cha robo ya kwanza cha Baraza la Wafanyabiashara wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino leo tarehe 24 Oktoba, 2024 kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri.1
Akichangia hoja ya ujenzi wa soko na stendi ya magari katika Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino, Mwenyekiti wa wafanyabiashara wa Wilaya ya Chamwino Bw. Richard Mmasi, ameshauri wataalam wanaoratibu ujenzi wa mradi huo kuhakikisha soko na stendi vinajengwa sehemu moja ili kuvutia watu wengi zaidi ambapo itasaidia kuwa na mzunguko mkubwa wa biashara na kuleta tija na hoja hiyo iliungwa mkono na wajumbe katika baraza hilo.
Akiunga mkono hoja hiyo ya ujenzi wa soko na stand, Mkuu wa Wilaya ya Chamwino Mhe. Janeth Mayanja ameshauri mradi huo licha ya kujengwa mahala pamoja lakini pia kujengwa karibu na makazi ya watu ili kuondoa kero ya Wananchi kufuata huduma hizo za soko na stand kwa umbali mrefu ambapo itasaidia mradi huo kuwa na tija kwa kupata watumiaji.
Sanjari na hilo, Mhe. Mayanja ambaye alikuwa Mwenyekiti wa kikao cha baraza hilo amewapongeza wajumbe waliohudhuria kikao hicho kwa kutoa ushauri na mapendekezo yenye manufaa zaidi kwa wananchi wa Wilaya ya Chamwino.
Aidha, Katibu wa kikao hicho na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino Ndg. Tito .P Mganwa amewahakikishia wafanyabiashara kuwa zoezi la upimaji wa ardhi linaendelea kwa kupima maeneo ya vipaumbele kwa ajili ya makazi , viwanda na biashara ili kuwa na mji uliopangwa na kuepuka ujenzi holela.
Kwa upande wa Afisa Biashara wa Mkoa wa Dodoma Bi. Mwajabu Nyamkomola, amepongeza hali ya kuimarika kwa mabaraza ya wafanyabiashara mkoa wa Dodoma tofauti na yalivyokuwa huko nyuma, sambamba na kumpongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kutambua umuhimu wa sekta binafsi katika kukuza uchumi wa nchi.
Aidha, amewasihi wafanyabiashara kuchangamkia fursa za utalii zinazopatikana katika Wilaya ya Chamwino ikiwemo historia muhimu ya vijiji vya ujamaa vilipoanzishwa katika Wilaya ya Chamwino ambapo itavutia watu wengi kuja kujifunza na kukuza utalii.
Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino
Sanduku la posta: 1126 Dodoma
Simu ya Mezani: 026 296 1511
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@chamwinodc.go.tz
Hakimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino. Haki zote Zimehifadhiwa.