Mkuu wa Wilaya ya Chamwino Mh. Janeth Mayanja leo tarehe 23 Januari, 2025 amehimiza mpango wa upatikanaji wa chakula kwa wanafunzi wote wa shule katika Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino.
Mh. Janeth Mayanja amehimiza mpango huo wakati akiendesha kikao cha lishe cha robo ya pili Oktoba hadi Desemba 2024 kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri.
Katika kutekeleza mpango huo DC Mayanja amewataka Maafisa Tarafa, Watendaji wa Kata na Vijiji katika Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino kutambua kata na vijiji ambavyo shule zake wanafunzi hawapati chakula muda wa shule ili nguvu kubwa iweze kuelekezwa katika maeneo hayo kwa kufanyika vikao na wazazi ili kutatua changamoto hiyo.
Sambamba na hilo, Mh. Mayanja amelishukuru shirika lisilo la kiserikali la Save the Children kwa kutoa mbuzi katika maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Chamwino wanaotumika kwa kuzalisha maziwa kwa ajili ya lishe ya watoto chini ya umri wa miaka miwili na hivyo kuwaomba kupeleka na mbuzi hao katika ngazi za shule ili wanafunzi wa madarasa ya awali waweze kunufaika na maziwa lishe hayo.
Aidha, DC Mayanja amewataka Maafisa tarafa, Watendaji wa Kata na Maafisa Kilimo kwenda kuwaelekeza Wenyeviti wa vijiji na vitongoji kuwaambia Wananchi katika maeneo yao kupanda zao la mtama kwa siku zilizobaki ili kukabiliana na hali ya upungufu wa mvua.
Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino
Sanduku la posta: 1126 Dodoma
Simu ya Mezani: 026 296 1511
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@chamwinodc.go.tz
Hakimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino. Haki zote Zimehifadhiwa.