Afisa Elimu Msingi wa Wilaya ya Chamwino Bi Zaina Ramadhan Kishegwe ametoa maagizo kwa wakuu wote wa shule za msingi Wilaya ya Chamwino kusimamia ufundishaji na kuhakikisha mahiri (mada) zote za darasa la saba zinafundishwa kikamilifu na kukamilika kabla wanafunzi hawajafanya Mtihani wa Taifa wa darasa la saba mwaka 2025.
Maagizo hayo yametolewa leo Novemba 5, 2024 katika kikao cha tathmini ya matokeo ya mtihani wa darasa la saba 2024 Wilaya ya Chamwino kilichofanyika katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri.
Bi Zaina Kishegwe ametoa maagizo hayo mbele ya wakuu wa shule za msingi Wilaya ya chamwino akiwataka kusimamia mahiri zote za darasa la saba kwa wahitimu wa mwaka 2025 na kuhakikisha kuwa zinakamilika kabla au ifikapo mwezi August mwakani ili wanafunzi wapate muda mzuri wa kujiandiaa kwa ajili ya mtihani wa Taifa wa darasa la saba wa mwaka 2025. Lengo ni kuhakikisha kuwa wanafunzi wa darasa la Saba wanafanya Mtihani wa Taifa wakiwa wamefundishwa kikamilifu ili kuongeza ufaulu.
Sambamba na hilo, walimu wakuu wameagizwa kuhakikisha wanafundisha madarasa ya mitihani ikiwemo darasa la saba ili kuonesha mfano kwa kutoa matokeo chanya kwa wanafunzi hali itakayoleta morali kwa walimu wengine pamoja na kuwataka wakuu wa shule hizo za msingi kuhakikisha wanafunzi wote katika shule zao wanapata chakula cha mchana shuleni.
Aidha, Bi Kishegwe amehimiza walimu wakuu kuwa na mahusiano mazuri na walimu wao pamoja na kuwaomba kutoa motisha hali itakayopelekea kuongeza morali kwa walimu na kupelekea mazingira mazuri ya ufundishaji shuleni.
Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino
Sanduku la posta: 1126 Dodoma
Simu ya Mezani: 026 296 1511
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@chamwinodc.go.tz
Hakimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino. Haki zote Zimehifadhiwa.