Kuelekea zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la kupiga kura katika Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino maafisa waandikishaji wasaidizi ambao pia ni watendaji wa kata za Wilaya Chamwino wamepatiwa mafunzo mbalimbali juu zoezi hilo.
Akizungumza wakati wa mafunzo hayo katika ukumbi wa mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino Septemba 18,2024 afisa muandikishaji wa Majimbo ya Chamwino na Mvumi Ndugu Godfrey Mnyamale amewataka maafisa hao wasaidizi kuzingatia mafunzo hayo kwani wataisadia tume katika usimamizi wa zoezi la uandikishaji katika vituo vyao, pia kutumia uzoefu wao na mafunzo waliyopatiwa kufanya kazi kwa weledi na bidii ili kufanikisha zoezi hilo.
Mnyamale ameeleza pia wakati wa zoezi hilo la uboreshaji wa daftari la kudumu la kupiga kura mawakala wa vyama vya siasa wataruhusiwa kuwepo katika vituo vya kuandikishia wapiga kura kwani jambo hilo ni muhimu kusaidia kuleta uwazi katika zoezi zima na mawakala hao watasaidia kutambua waombaji katika eneo husika ili kuondoa vurugu zisizo za lazima.
Amewasisitiza pia maafisa waandikishaji hao wasaidizi kutekeleza majukumu yao kwa umakini katika kila eneo ikiwemo utunzaji wa vifaa vya uandikishaji (BVR) kwani vifaa hivyo vitatumika pia katika maeneo mengine nchini katika zoezi la uandikishaji pia kuzingatia maelekezo yote yaliyotolewa na tume ili kuyafanyia kazi wakati zoezi litakapokuwa limeanza.
Aidha, zoezi la uboreshaji wa daftari la kudumu la kupiga kura katika Wilaya ya Chamwino litafanyika katika vituo 805 katika majimbo ya Chamwino na Mvumi kuanzia tarehe 25 septemba hadi tarehe 1 oktoba, mwaka 2024.
Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino
Sanduku la posta: 1126 Dodoma
Simu ya Mezani: 026 296 1511
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@chamwinodc.go.tz
Hakimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino. Haki zote Zimehifadhiwa.