Awataka Wananchi wa Chamwino Kujiunga na Mfuko wa Afya ya Jamii wa CHF Iliyoboreshwa.
Mkuu wa Wilaya ya Chamwino Bi. Vumilia Nyamoga amesikitishwa na tabu wanayoipata wananchi wa Chamwino katika huduma ya Afya kutokana na kukosa fedha wanapougua.
Ametoa masikitiko hayo akizungumza na wananchi wa kijiji cha Chiboli kwenye mkutano uliofanyika tarehe 03.07.2019 wenye lengo la kuhamasisha wananchi kujiunga na CHF ili wapate matibabu kwa gharama nafuu ya shilingi 30,000 kwa mwaka mzima pindi wanapougua wao na wategemezi wao.
Ndipo alijitokeza Charles Pongolo mkazi wa kijiji cha Chiboli na kusimulia adha aliyoipata alipouguliwa na mtoto wake na kutumia gharama kubwa za matibabu huku akitoa wito kwa wanakijiji wenzake kujiunga na CHF kabla hawajapatwa matatizo kama yaliyomkuta yeye.
"Najua huyu ni mmoja tu aliyezungumza hapa mkutanoni, lakini wapo wengi huuza mifugo, mazao hata nyumba pindi wapouguliwa. Naomba wananchi wa Chamwino tujiunge na CHF iliyoboreshwa ili tuwe na uhakika wa matibabu ya gharama nafuu." Alisema Bi. Nyamoga.
Aidhaa Mganga Mkuu wa Wilaya Chamwino Dkt. Asteria Mpoto amewaeleza wananchi kuwa kwa gharama ya 30,000 wanaweza kutibiwa kwenye ngazi zote za matibabu kwa kupata rufani kuanzia zahanati mpaka hospitali za rufaa tofauti na ilivyokuwa awali. Pia amewaeleza kuwa mwenye kadi ya CHF anaweza kutibiwa kwenye mikoa mingine ya Shinyanga, Manyara na Morogoro na serikali ipo kwenye mchakato wa kuwezesha mwachama wa CHF wa Chamwino atibiwe popote pale nchini.
Nae Afisa Maendeleo ya Jamii wa Wilaya ya Chamwino Bi. Asha Vuai amewaeleza kuwa wanachama wa CHF wanayofursa ya kujiunga na VIKOBA ili kujipatia mikopo ya kuendeleza shughuli zao za maendeleo.
Katika ziara hiyo Mkuu wa Wilaya amesikiliza kero mbalimbali kutoka kwa wananchi na kutoa maagizo kwa watendaji wa serikali kuzipatia ufumbuzi haraka.
Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino
Sanduku la posta: 1126 Dodoma
Simu ya Mezani: 026 296 1511
Simu ya Mkononi:
Barua Pepe: ded@chamwinodc.go.tz
Hakimiliki©2017 Halmashauri ya Wilaya ya Chamwino. Haki zote Zimehifadhiwa.